NJAMA - 3

NJAMA - 3

Author:
Price:

Read more

NJAMA - 3




Simulizi : Njama
Sehemu Ya Tatu (3)

Kutokana na maelezo ya huyu mtu nikajua anasema kweli. Nilijilaumu kumwua Kimkondo maana yeye huenda angetupa mwanga zaidi. Lakini hii yote inaonyesha jinsi majahiri hawa yalivyokuwa yamepanga ujahili wao kwa ufundi.

"Lo Willy asante sana".

"Sahau", nilimjibu kwa mkato.

Ile sura ya kikatili ilikuwa tayari imekuja usoni mwangu. Katika hali kama hii sura yangu hubadilika na kuwa mtu tofauti kabisa. Hivyo nilipomwambia Sherriff sahau niliona anashituka kidogo.

"Twende zetu tutoke hapa Sherriff, huyu nitajua mahali ya kumpeleka".

Tulimtangulia, tukafungua mlango wa bohari tayari kurudi mjini. Tulipokuwa tumefika kwenye kona niliyotokea, tukasikia honi ya gari ya namna ile ile waliokuwa wamepiga hawa majahili wa kwanza.

"Sherriff na wewe mtu mjifiche nyuma ya hili gari, kwa vile mimi nimevalia koti lao ambalo naona ndicho kitambulisho chao nitakwenda kufungua lango, unayo ile bastola uliyochukua kwake?".

"Ndio".

"Basi akifanya ushenzi unajua la kufanya; maiti hazisemi'.

Niliwaacha nikakimbia mpaka kwenye lango nikafungua. Gari aina ya VW Kombi iliingia imejaa watu wamevalia makoti kama langu, Gari hili lilisimama nyuma ya lile gari la kwanza. Milango ikafunguliwa wakaanza kutoka. Mimi nilikuwa tayari na SMG yangu.

"Rudini ndani......." niliona yule mtu tuliyekuwa tumemshika ameruka juu ya gari na kutoa onyo, lakini kabla hajamaliza Sherriff alimlamba risasi ya kichwa akaanguka juu ya gari, mimi nikajua tayari mambo yametibuka, hivyo sasa ni kazi.
Dereva wa gari hii na watu wengine waliokuwa bado ndani ya gari walifunga mlango ili waondoke. Wale waliotoka nje walianguka chini na kutoa bastola tayari kwa mapambano. Mimi nilikuwa nimeishavua koti nimerukia ukutani na tayari SMG mkononi. Nilikuwa nimelalia tumbo juu kabisa ya ukuta. Lile gari lilipopiga moto, nililenga mlango wa dereva na kuachia risasi mfululizo kama mchezo.

Sherriff alikuwa bado kimya hajaanza shughuli. Wale watu watano waliokuwa wametoka ndani ya gari nao walikuwa wametambaa upande mwingine wa kombi. Kumbe mmoja wao aliniona kule juu baada ya kuona risasi zilizoua wenzake zikitokea juu. Mimi nilikuwa bado sijamwona hivyo akainuka kunimaliza. Lakini kumbe Sherriff alimwona kabla hajafyatua risasi, akamwahi. Nilipomwona Sherriff akanionyesha ishara. Alikunja kiganja halafu akainua kidole kimoja kuonyesha kuwa ni watano na mmoja tayari kafa.

Mimi nilijirusha chini toka ukutani na kujiviringisha huku nakoswa koswa risasi za maadui. Niliposimama huku nikikimbia zigizaga na wakati huo nikipiga risasi ovyo kuwazuia wasipige. Nilifika mlango na kufungua kama ninakimbia nje. Wale kwa woga wao walipoona hivi nao walianza kukimbia kuwahi mlangoni.

Kumbe ndipo walikuwa wanampa fursa Sherriff kuwachukua mmoja mmoja vizuri sana. Na mimi ghafla nilijitokeza tena na kumimina risasi kwa wawili waliokuwa mbele. Bahati nzuri Sherriff alijitupa chini la sivyo ingetokea ajali kwani yeye alifikiri nitawasubiri nje hivyo naye alikuwa anawafuata nyuma.

"Kazi nzuri Sherriff, la sivyo ningekuua, pole sana", nilimpa mkono.

"Hali kama hizi nimezizoea sana hivyo huwa niko tayari katika tahadhari kila mara kwani lazima kama huna uhakika mwenzako atafanya nini baadaye tegemea lolote", Sherriff alijibu.

Tulikimbia kutoka pale mpaka kwenye gari langu. Tuliingia na kuwasha gari moto na kuelekea zetu mjini.

"Mimi nilijua ndio mwisho wangu", Sherriff aliniambia.

"Kwa nini?".

"Maana walivyonivamia hata nilishindwa la kufanya halafu nilijua wewe utakuwa unanisubiri New Afrika na kumbe mimi nimeshauawa. Na kweli wangeniua".

Alitoa shati lake kuonyesha uvimbe mbaya sana kwenye tumbo lake.

"Nasikia maumivu ya ajabu. Watu hawa ni katili sana".

"Pole sana. Jambo la kusikitisha ni kwamba imebidi tuwaue wote. Hivyo bado tumerudi pale pale; hatujui lolote, isipokuwa tu kwamba watu hawa ni majahili wa hatari sana wanaovaa makoti mekundu na bunduki wanazotumia ni SMG za kichina, bastola za kirusi zenye sailensa. Zaidi ya hapo bado tuko mbali sana na ukweli wa mambo. Ila kinachonifurahisha ni kwamba sasa watashtuka baada ya mapambano haya ambamo tumeua watu wao karibu kumi na tano. Kule kushtuka ndiko kutatusaidia maana lazima watahaha na kufanya makosa".

"Sawa kabisa. Lakini mimi nataka kujua jinsi ulivyojua nimekamatwa na namna ya gari umeweza kuniokoa. Maana mimi sikuamini nilipokuona, nilidhani huenda ni malaika kashuka toka mbinguni katika sura yako".

Tukiwa bado tunaelekea mjini nilimweleza jinsi nilivyofanya.

"Lo ndio sababu wewe ni mpelelezi namba moja katika Afrika; mimi sasa nadhani hata katika dunia. Tukirudi London salama nitailisha komputa maelezo zaidi juu yako tuone itakuonyesha katika nafasi gani katika wapelelezi wa ulimwengu".

Mimi nilicheka tu sikujibu kitu.

"Na kule kubadili gari kulisaidia sana maana walipochungulia na kulikosa gari lako walinidhihaki kwa kusema kuwa sasa nitakufa peke yangu hata rafiki zangu hawatathubutu kuja hata kama wangeniona wakati ninakamatwa".

"Mimi ni mjuzi zaidi yao; lazima tuzidiane maarifa".

Tuliingia barabara ya Independece Avenue.
"Nitakupeleka kwa daktari wangu hapa Zanaki Street, na utalala hapo. Nafikiri kesho utakuwa katika hali nzuri, kwa leo lala hapo usirudi New Afrika ili daktari aweze kukupa matibabu kwanza. Nitakuja kukupitia asubuhi".

"Sawa wewe ndiye bosi", Sherriff alijibu.

Nilimpeleka kwenye zahati ya rafiki yangu Dk. Kiluwa na kumweleza amtibu na malipo yatalipwa na AIA. Nilimwacha nikawaahidi kuwaona asubuhi yake.

"Eddy nafikiri unaweza kwenda kupumzika. Acha vijana wa zamu waendelee, maana kesho tunaweza kuwa na kazi nyingi sana".

"Asante tutaonana asubuhi", alijibu huku akikusanya kusanya karatasi zake.

Mimi niilimuaga nikaondoka zangu kuelekea New Afrika tayari kuonana na Veronika. Nilipofika New Afrika nilikuta duka la kahawa limejaa watu na ile sehemu ya Patio Baa ndio usiseme, maana vijana walikuwa wamejazana wakifurahia saa zao za baada ya kazi.

Nilishikashika mfukoni, nikachukua funguo za gari mkononi nikaelekea kwenye gari langu, niliona Vero alikuwa bado hajafika kwani hamkuwa na mtu ndani ya gari. Nilifungua mlango wa upande wa dereva ili nikae nimsubiri, maana nilijua asingechukua muda mwingi.

Nilipoingia na kukaa kitini na kuanza kutelemsha kioo, nilisikia kama kuna kitu kwenye viti vya nyuma vya gari langu. Nilipotaka kugeuka kuangalia nilisikia sauti ikisema. "Usigeuke la sivyo utakuwa ndio mwisho wako. Washa gari ondoka, na ufuate maelezo yangu".

Nilisikia mdomo baridi wa bastola ukigusa shingo yangu.

"Sawa mzee", nilijibu huku nikijifanya kama sijali.

"Siyo mzee, sema wazee. Tuko wawili na wote tuna bastola na tunajua kuzitumia hivyo usijaribu kitu chochote cha kuleta matatizo".

"Mimi sina wasiwasi, maana sijui kwanini natekwa nyara, kama nia yenu ni gari niambieni niwaachie. Mimi ni mfanyabiashara nitapata gari nyingine, kwangu pesa si tatizo".

"Funga domo lako, sisi hatuna haja na gari lako wala pesa yako, sisi tuna pesa kuliko wewe".

Kabla sijasema lolote aliniambia. "Kata kushoto ingia Independence Avenue, halafu ukifika 'Clock Tower' ingia mtaa wa Railway halafu shika barabara inayopita kwenye kituo cha polisi wa usalama barabarani, halafu ukifika kwenye mzunguko ingia kushoto, fuata barabara ya Kilwa mpaka nitakapo kueleza tena. Nasema tena ujanja wowote utakutokea puani".

"Usiwe na wasiwasi", nilijibu kiume.

"Nyamaza", alijibu kwa sauti ya ukali.

Nilijilaumu sana kwa kutochukua tahadhari zaidi kwa watu hawa.

Nilifikiria kama naweza kufanya lolote sasa nitakuwa kwenye upande wa hasara hivyo nikakata shauri la kufuata maelekezo mpaka mwisho ndipo nione la kufanya. Maana nafikiri kama nia yao ilikuwa ni kuniua wasingesita, walikuwa na mwanya mzuri sana nilipoingia bila tahadhari ndani ya gari. Nilijua nia yao si kuniua ila kuna habari walizozitaka. Nilimfikilia Veronika nikajua atahangaika sana kwani hatanikuta halafu hatajua Sherriff aliko.

Tulipokaribia uwanja wa Sabasaba aliniamuru nikate kushoto kwenye njia inayoelekea kwenye ofisi mojawapo za reli ya Tazara ya Kurasini. Tulipotelemka kidogo aliniamuru nikate kulia na kuingia kwenye mlango wa pembeni wa uwanja wa Monyesho ya Sabasaba.

Tulipofika kwenye mlango huu aliniamuru nipige honi. Nilipopiga honi mlango ulifunguliwa. Taa zangu zikamwulika mlinzi aliyevaa joho jekundu, nikajua mara moja ni nani nimepambana nae tena. Tena huyu mtu aliongeza na kofia nyekundu juu.

Nilishangazwa sana na mbinu za watu hawa, maana sehemu zo walizokuwa wanazitumia kama kambi zao za kufanyia uovu zilikuwa sehemu za kiserikali. Hii ilionyesha jinsi mbinu za watu hawa zilivyozidi kiwango.

"Ingia ndani moja kwa moja, fuata barabara mpaka nitakapokuabia simama", niliamriwa.

Uwanja ulikuwa kimya kabisa. Giza lilitanda kote ila taa za gari langu peke yake. Tulikwenda mpaka katikati ya vibanda.

"Simama hapa, zima taa na telemka taratibu. Ukifanya makosa usinilaumu", alinieleza. Nilipozima taa tu niliona vivuli vya watu vikinyata polepole kuja kwenye gari. Nilipokanyaga nje tu gari likawa limezungukwa na watu watatu. Wale waliokuwa ndani ya gari walitelemka.

"Mmemleta?", mmoja wa wale waliozunguka gari aliuliza.

"Ndio", alijibu yule mtu aliyekuwa ananipa amri".

"Kazi nzuri, haya twendeni".

Yule mtu aliyezungumza alitangulia mbele mimi nikaambiwa nimfuate huku nimezingirwa na watu wanne. Yaani wale wawili walioniteka, na wengine wawili waliokuwa wamebeba bunduki aina ile ile ya SMG, ilionekana hawa watu walitumia sana aina hii ya bunduki.
Niliongozwa moja kwa moja mpaka kwenye kibanda kimoja katikati kabisa ya uwanja wa maonyesho wa Sabasaba. Nilikumbuka kuwa kibanda hiki kilikuwa kinatumiwa na nchi za Zambia katika maonyesho ya Kimataifa. Mlango ulifunguliwa tukaingia. Ndani tulimkuta mtu mwingine anavuta mtemba amekaa kwenye kiti huku akitabasamu. Watu hawa wote walivalia majoho mekundu. Na hawa wanne niliowakuta huku kiwanjani walivaa kofia nyekundu isipokuwa wale walioniteka ndio hawakuwa na kofia.

"Karibu Willy Gamba, keti chini kwenye kiti", aliniambia yule mtu tuliyemkuta ndani.

"Asante, mimi ningependa kusimama", nilijibu.

"Mimi sitaki kukukarisha kwa nguvu, lakini kama unaona ni lazima nifanye hivyo ninao uwezo, Willy", aliniambia taratibu huku wale watu wengine wakinisogelea. Niliona hakuna haja kuchachamaa hapa hivyo niliketi kwenye kiti.

Chumba hiki kilikuwa kimewekwa fenicha nzuri sana, hata nikashangaa saa ngapi watu hawa waliweza kuaandaa chumba hiki kama ofisi na huku uwanja huu siku zote unalindwa.

"Romano na Charles mnaweza kwenda nje kusudi muwe tayari kukabiri jambo lolote linaloweza kutokea hapo nje wakati nikiwa na mazungumzo mafupi na Willy hapa", alitoa amri polepole kiasi kwamba ungeweza kuamini kuwa ni mtu mzuri sana, lakini macho yake yalionyesha uovu usio kifani.

NIlifurahi sana kwani nilijua kuwa sasa ninaonana na mtu wa maana katika kundi hili la majahili. Macho yetu yalipokutana ana kwa ana mara moja tukatambuana, maana huyu alikuwa jasusi wa hali ya juu. Sisi tuko kama mbwa tunajuana kwa harufu. Wale watu wawili wenye SMG walitoka nje tukabaki na wale watu walioniteka nyara, yule mtu aliyetupokea na huyu mtu tuliyemkuta humu ndani. Walipotoka nje waliufunga mlango.

"Bwana Gamba, mimi ni mtu nisiyependa kuumiza kwa sababu mimi huwa sijisikii vizuri nikiona mtu anaumizwa. Lakini nikilazimika kufanya hivyo, basi mimi hufumba macho. Nisingependa nifumbe macho kwako kwa hiyo naomba sana uwe mtu mwungwana katika kujibu maswa yangu".

"Nadhani ungependa kujua sisi ambao tuko hapa ni nani, sisi ni WANAMAPINDUZI WAPINGA MAPINDUZI".

"Wanamapinduzi wapinga mapinduzi maana yake nini?. Sikuelewi.

"Ni kwamba sisi tunapinga watu wanaojiita Wana mapinduzi, wanaofikiri wataleta uhuru Afrika Kusini kwa njia ya vita. Sisi ni wanamapinduzi ambao tuna imani kuwa tutaleta uhuru Afrika Kusini kwa mazungumzo bila kuua mtu hata mmoja. Sasa swali langu ni hili; Wewe na rafiki zako mna nia gani katika kupeleleza upoteaji wa silaha?, Kwanini msiwaachie watu wanaohusika?".

"Mimi si mwana siasa hivyo unayonieleza juu ya namna gani uhuru utakavyopatikana huko Afrika Kusini sina haja ya kujua. Lakini wageni wangu ni waandishi wa habari na kumetokea hapa mjini Dar es Salaam wizi wa silaha uliotingisha ulimwengu.Hivyo wakiwa waandishi lazima wapeleleze wapate kueleza ulimwengu mambo haya yametokeaje. Sidhani kama kitu hocho ni dhambi. Ni kitu cha kawaida". Nilimjibu taratibu nikijaribu kupima hali ndani ya chumba hiki.

"Imeonekana hawa waandishi wa habari wamekwenda zaidi ya kiwango cha upelelezi wa kigazeti, kiasi cha sisi kuamini kuwa si waandishi wa gazeti ila wapelelezi. Jioni hii kama huna habari rafiki yako Sherriff ameua vijana wangu zaidi ya kumi. Mtu mmoja, Willy, mtu mmoja?, siamini kabisa kuwa yeye ni mwandishi".

"Swali langu la pili nataka nujue yeye ni nani na sasa hivi yuko wapi?. Ukijibu maswali haya nitakuachia, usipojibu jua ya kwamba kesho huioni".

"Mimi ninavyojua ni kwamba yeye ni mwandishi wa habari, kama ni mpelelezi haya ni maneno yako, Kampuni yangu ni wakala, hivyo nilivyofanya mkataba na gazeti la Afrika na watu hawa walipokuja nilijuwa ni waandishi. Pili sijui aliko sasa hivi, tuliachana saa nyingi na tulipanga tuonane saa kumi na mbili New Afrika Hoteli lakini sikumkuta.

Baada ya kufikiri kidogo akasema, "La hasa, unajua".

"Sijui".

"Au unataka mpaka nifumbe macho".

"Hata kama ukifumba macho, sijui".

"Lucas na Moshi hebu mmwonyesheni huyu namna ya kujibu", alisema tena pole pole.

"Simama", alisema Lucas.

Sikusimama. Basi walinijia wote pale kitini kama faru, na mimi Willy tayari nilikuwa nawashwa kumwonyesha huyu mkubwa wa kuwa Willy hasukumwi ovyo.

Kama umeme nilisimama upesi na kukwepa ngumi ya Lucas na kwa sababu alikuwa ameitupa kwa nguvu sana alipepesuka mimi nikampiga teke kwenye mapumbu akalia kama nguruwe na wkati huo shoto langu lilimfikia Moshi singoni nae akapepesuka mpaka chini. Yule mtu mwingine aliyetuongoza toka mwenye gari alitoa bastola yake lakini mimi niliona hatua hiyo nikaruka upande mwingine wa chumba na risasi zikanikosa, na wakati huo mlango nao ulifunguliwa na mtu aliyevaa joho jekundu na kofia nyekundu akiwa na SMG mkononi akampiga risasi ya mgongo kabla hajanimaliza pale niliporukia, na yule mtu akafa pale pale. Huyu mtu wa SMG alimimina risasi kwa wale wengine waliokuwa wanajaribu kutoa silaha zao na kuwamaliza hapo hapo. Mimi katika harakati za kujiokoa niona yule mkubwa wao anaruka nyuma ya kiti, nikatoa bastola yangu, lakini nikawa nimechelewa, kwani nyuma ya kiti chake kulikuwa na mlango mdogo kimo cha urefu wa kochi. Hivyo alijitumbukiza.
"Anaondoka huyo Willy", nilisikia sauti nya Veronika akimimina risasi pale kwenye mlango lakini yule mtu alikuwa anajua nini anachofanya, hazikumpata akakimbia nje.

Mimi nilishangaa sana kumwona Veronika katika joho jekundu na kofia nyekundu na SMG mkononi amefika wakati kabisa uliohitajika kuniokoa.

"Oh Vero mkombozi wangu, umetokea kama malaika vile".

Alitupa bunduki akavua kofia na joho, haraka hara akaja akanirukia shingoni na kuanza kunibusu, kisha akaniachia.

"Tutoke hapa mpenzi, nitakueleza baadae", alininong'oneza.

Tulitoka ndani ya banda hilo na kusikia gari linaondoka.

"Mshenzi amepona", Veronika alisema.

"Iko siku yake", nilijibu.

Niliokota bunduki mbili pale nje. tukaenda kwenye gari letu tukaziweka ndani. Tukawasha gari na kuelekea mjini. Tulipofika Kilwa Road Veronika alianza kunisimulia,


CHIMALAMO

"Baada ya kuzungumza na wewe kwenye simu, niliondoka kwenda New Afrika kama tulivyoagana. Niliona hakuna sababu ya kuchukua gari, hivyo niliondoka kwa miguu kwani nilijua dakika kumi ningenitosha. Nilikuja moja kwa moja na barabara ya Azania Front nikakatisha pale kwenye kanisa la Kilutheri na kutokea barabara ya City Drive. Kama unavyojua New Afrika inajengwa kwa mbele kwa hivyo nilijipenyeza kwenye mwanya wa jengo la Benki ya Taifa ya Biashara tawi la City Drive na Azikiwe, nikawa nimetokea karibu kabisa na pale ulipoegesha gari lako".

Ghafla nikaona watu wawili, mmoja wao akifungua mlango wa gari lako. Mimi nikasimama na kujibanza kwenye moja ya nguzo za jengo hili la Benki huku giza likinisaidia. Yule wa mbele aliingia na nyuma akaangalia huku na huko hakuona kitu nafikiri, maana alitoa bastola mwenye joho lake nae akaingia. Kama unavyojua gari hili lina milango miwili tu, hivi waliinamisha kiti na kuingia nyuma ya gari.

Mara moja nikajua nia yao; nilijua wanakusubiri wewe ama kukuua ama kukuteka nyara. Nilipofikiri sana niliona nia yao kukuteka nyara kwani kama ni kukuua wasingeingia ndani ya gari, hasa nyuma, na mahali penyewe pakiwa karibu sana na New Afrika. Huwa naamini sana akili zangu zinavyonituma hivyo nikaona kuwa nia yao ni kukuteka nyara. nilifikiri nikufuate lakini sikuwa najua ofisi yako ilipo. Hivyo nikaamua kitu kimoja, kuingia ndani ya buti la gari kama iwazi. Kwa kuwa gari yako ina nyavu kioo cha nyuma, nilijua watu hawa hawataniona wala kunisikia, kwani nilijua na wao watakuwa wamelala chini ili usije ukawaona wakati unaingia".

Alinyamza kidogo ili kulegeza koo kwa mate, akaniangalia akanikuta mimi naendesha taratibu huku nikimsiliza kwa makini sana. Kisha akaendelea, "Nikisaidia na giza la ukuta wa mabati uliozungushiwa jengo hili la mbele la New Afrika huku nikinyata nimeinama kimo cha buti la gari. Kama bahati ilivyokuwa na mimi nilikuta buti lako halikufungwa na funguo. Jihadhari sana siku nyingine utabeba adui ndani ya gari lako".

"Nimekuwa sina aduin Tanzania, hivyo nimekuwa nikiamini kuwa hakuna mtu wa kunifanyia ubaya, maana hata sijawahi kugombana na mtu hapa Dar es Salaam".

"Haya sasa lazima utambue kuwa umepata maadui; lazima ujihadhari".

"Sawa nitajihadhari lakini vile vile kama ningekuwa nimefunga usingeweza kuniokoa, hivyo kujiachia mambo mara nyingine ni vizuri".

"Haya nimekubari kushindwa, lakini hata hivyo ningepata njia nyingine. Basi taratibu nilifungua buti la gari na kuingia ndani, kimya kimya kabisa bila kelele yoyote. Niliwahi kusafiri ndani ya buti wakati ninakaa na majeshi ya POLISALIO, hivyo najua sana hali ilivyo ndani ya buti la gari kiasi kuwa kwangu hewa ya mle ninaweza kuistahamili ingawa ni kidogo. Unajua gari linapoanza kutembea hewa inajaa kabisa. Basi baada ya kuingia na kulifunga kinamna, kiasi ambacho lisingeweza kunishinda kufungua, baada ya kuliangalia kufuli lenyewe.
"Muda si mrefu nilisikia mlango unafunguliwa; unajua hili gari lako lilivyoundwa ukiwa ndani ya buti unasikia maneno yanayozungumzwa ndani ya gari. Basi niliwasikia wakikuamrisha kuendesha gari ndipo nikajua nilivyohisi ni sawa. Ulipopiga honi na kusimama kama ulivyoamrishwa, nilijua tunaingia mahali na nikajua kuna mtu anayefungua na kufunga mlango ni wa kundi lao hivyo atakuwa ni mlinzi mwenye silaha.

"Tulipoanza kuondoka niliinua mlango wa buti kidogo sana na nikamuona mtu huyu nusu amebeba bunduki. Niliendelea kuchungulia hivi hivi nikaona njia tuliyotokea kutoka kwenye lango mpaka gari liliposimama nikabana tena mlango. Nikasikia wanakuamru toka kisha nikasikia sauti zingine hapo nje halafu pakawa kimya, ndipo nikafungua taratibu mlango na kutoka nje. nikakata shauri lazima nipate silaha ili niweze kukuokoa.

"Hapo ndipo nilipoanza kurudi mbio kwenye lango ili nikamnyanganye silaha yule mlinzi. Nilipokaribia lango nilimuona yule mlinzi amesimama anavuta sigara huku anaangalia upande wangu. Nililala chini na kusubiri. Alipogeuka na kuangalia upande mwingine nilianza kutambaa chini kimya kimya. Nilikuwa nimefundishwa na wanajeshi wa Polisalio namna ya kumnyemelea mtu kwenye giza bila yeye kushituka. Nilipokuwa karibu nae kabisa, nilisimama na kupiga kelele, "Yeeeeee".

"Alishituka na kuingiwa na hofu na kabla hajatokwa na hofu nilipiga teke mikono yake bunduki ikaanguka chini. Alipoona hivi akaanza kukimbia. Niliruka na kumpiga teke mgongoni akaanguka chini. Bila kuchelewa nilimrukia shingoni, ndivyo ikawa kwaheri. Nilimvua joho nikalivaa halafu nikatafuta kofia. Nilipoipata nikaivaa halafu nikachukua bunduki nikakuta ni aina ambayo wanaitumia wana mapinduzi wa Polisalio, yaani SMG ya kichina, hii bunduki niliitumia sana wakati nimekaa na hawa mashujaa wa Polisalio.

"Nilipoipata silaha hii, nilikimbia kurudi kwenye kibanda mlichoingia nipokaribia nikaona watu wawili wenye bunduki nikononi wakizunguza. Mimi nilizunguka nyuma ya kibanda cha karibu, halafu nikakohoa kisha nikazunguka haraka kutoka pale nilipokoholea. Nilisikia mmoja wao akisema; "Umesikia hicho".

"Ndio", alijibu mwenzake.

"Wewe zunguka huku na mimi nitapita huku".

"Hii ilinipa nafasi kujitayarisha, sikuwa nahitaji kutumia bunduki maana mrio ungewashitua watu waliokuwa ndani ya kibanda. Kwa vile nilikuwa nimevaa nguo kama wao na kofia, nilizunguka na kukutana na mmoja wao, yeye alinichukulia ni mwenzake shauri ya mavazi na giza. Tulikaribiana sana akabweteka; "Umeona nini?". Mimi niliinua mkono kumuonyesha nyuma yake na alipogeuka tu nikamkata karate ya shingo iitwayo ua na bila shaka alikufa pale pale. Nilimdaka haraka haraka na kumlaza chini bila kishindo. Kisha nikageuka upesi upesi ili nikutane na yule aliyepita upande mwingie sikuchukua hata hatua tatu tukawa tumekumbana hata yeye mavazi yalimdanganya na kufikiri mimi ni mwenzake.

"Huku hakuna kitu", aliniambia kwa sauti ya chini chini. Nilimdanganya kwa kumuonyesha kwa ishara aangalie nyuma yake na yeye akadanganyika. Hapo ndipo nilipomrukia nikamtia kabali ya hali ya juu mpaka niliposikia shingo linakatika nikamwachia. Sina mkanda mweusi wa judo na karate bure Willy, najua jinsi ya kuutumia".

"Zaidi ya ambavyo ningetegemea mrembo kama wewe kuutumia", nilimjibu huku nikitoa tabasamu.

"Asante. Baada ya hapo ndipo nilikimbia na kupiga teke mlango kwani nilisikia mlio wa bastola kabla sijapiga teke mlango. nilipoingia nilikuona chini hivyo nikafanya kama ulivyoona. Lo! Willy mpenzi niliogopa niliposikia mlio wa bastola nikafikiri wamekuua!".

"Si lahisi kuniua".

Nia yao ilikuwa nini?".

Nilimweleza yote waliyoniuliza.

Wakati namaliza kumweleza nilikuwa nataka kutoka barabara ya Upanga na kuingia nyumbani kwangu na kupeleka gari moja kwa moja gereji. Tukashuka nikafunga mlango wa gereji.

Karibu ndani vero.Hapa ndipo nyumbani kwangu".

Nilifungua mlango na kuwasha taa ya sebuleni halafu nikamkaribisha ndani akaketi kwenye
kochi.

"Asante lakini sitakaa sana, maana nasikia uchovu, nataka kurudi hotelini nikalale".

"Hakuna haja Vero nina mengi sana ya kukusimulia, maana hata sijakueleza yaliyotupata na Sherriff. Halafu....... nikasita kidogo".

"Halafu nini?", aliuliza kwa shauku.

"Halafu uliniahidi tulipokuwa Siera Leone kuwa tutafahamiana vizuri zaidi Dar es Saalaam, lazima ujuwe kwamba ahadi ni deni".

"Haya baba umeshinda".

"Asante".

Nilichukua vinywaji ndani ya barafu, halafu nikamkaribisha katika chumba cha kulala. Nilizima taa sebuleni nikafunga mlango wa mbele, nikakagua vyumba vyote vya nyumba pamoja na madirisha na milango. Nilipoona kila kitu ni salama nilirudi chumbani nikafungua mlango wa maliwatoni, nikajaza maji kwenye karai la kuogea. Nilimwita Veronika aje tuoge. Tulioga pamoja na mtoto huyu mara moja nikasahau matatizo yangu yote na uchovu wote wa jioni ile. Baada ya kutoka maliwatoni tulikuwa tayari kulala.

"Haya nieleze sasa wakati tukipumzika", Veronika alisema huku amelala karibu yangu.
Nilizima taa yenye mwanga mweupe, nikawasha yenye mwanga wa bluu. Nikaleta chupa yenye whiski kwenye meza ya kitanda nikammiminia Vero ndani ya glasi nikaweka mawe ya barafu na mimi nikatengeneza yangu.

"Na tunywe kwa usalama wa maisha yetu wote".

Tulianza kunywa huku nikimweleza yote yaliyotupata. Baadae tukaelezana mambo yetu binafisi ambayo yalitufanya tujishitukie tumekumbatiana na kubusiana.

"Amka", Vero alinishitua, "ni saa mbili sasa.

Nilimwangalia Vero ambae alionekana kuwa alikuwa ameamka kitambo kwani alikuwa na sahani ya mayai ya kukaanga na vikombe viwili vya kahawa. Alikuwa amevaa pajama zangu; alitoa sura ya kuchekesha, hivyo nilimcheka, maana zilimpwaya sana.

"Unapendeza katika pajama hizo", nilimtania.

"Kwenda huko".

Mimi nikaangua kicheko, nikatoka kitandani na kukaa.

"Mwenzangu umelala fofofo leo. Mimi nimeamka nikafanya mazoezi kisha nimekwenda jikoni nikatayarisha chochote. Haya tunywe kahawa utoe usingizi", alisema huku akikaa karibu nami.

"Mimi naona nikaoge kwanza".

"Hapana. Tunywe kahawa kwanza halafu tutafanya mazoezi ya judo na karate ili niwe katika hali nzuri, halafu ndipo tutakwenda kuoga".

Basi tulikunywa kahawa na mayai ya kukaanga, halafu tukatoka nje uani kufanya mazoezi. Nyumbaq yangu ilikuwa imezungukwa na ua mzuri wa michongoma iliyokatwa vizuri na yenye urefu wa futi saba. Hivi ukiwa uwani kwangu mtu anayepita nje ya ua hawezi kuona kitu chochote kinachofanyika ndani. Basi tulifanya mazoezi ya karate na judo ya hali ya juu sana. Hii ilinihakikishia kuwa Veronika alikuwan na ujuzi wa kutosha. Ilibidi tu kumwonyesha kuwa mimi najua zaidi nilipomwingizia staili nyingine za pekee ambazo hutumiwa na wajuzi wa hali nya juu katika karate na kung-fu kama mimi, ambazo zilimshinda kuzifuata.

"Ujuzi wako unatosha kabisa Veronika. Naamini unaweza kupambana na mtu yeyote, na nina imani ni watu wachache sana wanaweza kukushinda katika karate na judo".

"Asante kwa pongezi laki. Lo, lakini wewe mwenzangu ni zaidi. Mitindo mingine unayotumia sikuwahi kuiona hata kwa walimu wetu huko Japan. Ndio sababu wanasema ulipambana na Inoki na kutoka nae sare. Nilivyani walikuwa wanaongeza chumvi lakini sasa ninaamini ni kweli. Kokote nitakapotembea na wewe hata pakiwa ni pa hatari namna gani sitaogopa kabisa maana nina imani kubwa katika uwezo wako kwa jambo lolote sasa".

"Asante".

Baada ya mazoezi tuliingia pamoja maliwatoni tukakoga.

"Mimi itabidi unipeleke hotelini nikabadili nguo. Angalia hizi zilivgyochafuka kwa ajili ya matatizo ya jana usiku!".

"Usiwe na taabu, lolote utakalosema".

Mimi nilibadilisha nguo, nikavaa vizuri kabisa kama mfanyabiashara. Nilichukua silaha tulizokuwa tumeziteka nikaziweka sehemu yangu ya siri ambako huweka silaha zangu na ni mimi peke yangu ninayepajua mahali hapo. Na hata ukiwa mtu wa namna gani huwezi kupagundua. Nilichukua silaha nyepesi kwa ajili ya siku hiyo kama litatokea jambo lolote. Nilimpatia Veronika bastola yenya sailensa. Nilipoona mipango yote nimekamilisha tuliondoka kuelekea Kilimanjaro hoteli. Ilikuwa saa tatu na robo tulipofika Kilimanjaro.

"Nenda kajitayarishe, kabla ya saa nne mimi nitakuwa hapa".

"Utanikuta tayari", Veronika alijibu.

Niliondoka na kuelekea ofisini. Nilimkuta Eddy nae anaingia. Alipoona gari langu akasimama mlangoni kunisubiri.

"Habari za leo bosi?".

"Nzuri Eddy, umelala salama kijana?".

"Ndio, bila taabu".

"Twende ofisini kwangu". Tulielekea ofisini kwangu. Tulimkuta Linda anazungumza kwenye simu. Alipotuona akasema, "Huyu ameingia", Akanipa simu huku akisema "Maselina huyo.

"Halo mrembo, habari za asubuhi?".

"Nzuri tu, wasiwasi kwako ambaye unalala mpaka saa tatu na waandishi wa habari ".

"Mwongo, nani kakuambia huyo mwandishi kalala kwangu ?".

"Nani hakujui, danganya wengine lakini miye baba unajua kabisa kuwa nakujua kama nyuma ya kiganja changu".

"Haya umeshinda wewe".

"Njoo Chifu anakuhitaji, anataka kujua umefikia wapi mpaka sasa".

"Haya nakuja, nitamweleza mpaka yeye atachoka".

"Haraka basi", alisema Maselina na kukata simu.

"Eddy jambo lolote juu ya Kiki?".

"Si nilikwambia nitakuwa na habari zote saa nne, na saa nne bado". Eddy alijibu.

"Oke, je juu ya bohari la Mamlaka ya Pamba umepata nini?".

"Walinzi wote wa bohari hilo wamekutwa leo asubuhi wameuawa huko Temeke. Inaonekana walilichukua bohari hilo kwa nguvu ili wafanyie kazi zao kwa muda tu. Kila kitu kingine ni salama. Polisi wanashughulikia hayo ya jana na kujaribu kutambua maiti walizozikuta hapo. Wao wanafikilia ni wezi. Gari walilotumia nalo lilikuwa limeibiwa".

Kisha nikamweleza yaliyokuwa yametupata na Veronika, baada ya kuachana nae jioni ile.

"Sasa fanya uchunguzi ujuwe watu hawa wamejiingizaje huko uwanja ya maonyesho ya Saba Saba, maana uwanja huo unalindwa na polisi masaa ishirini na nne!.

"Nafikiri mtindo wao ni ule ule. Wanaua walinzi na kufanya makao ya muda. Wakimaliza shughuli zao wanakwenda kuteka mahali pengine lakini hata hivyo vijana watachunguza".

"Oke, ngoja mimi nikamwone Chifu halafu tutaanza upelelezi wetu, kama kawaida utatufuata toka New Afrika kama jana, sawa>".

"Bila wasiwasi bosi, kiijana ninayefuatana nae ni mzuri sana nafikiri hata nyinyi mlitupoteza".

"Ndio, kazi yenu ya jana ilikuwa nzuri sana, nilimpongeza.

"Bossi unapendeza sana leo".

"Asante sana kwa pongezi lako. Ngoja nikamwone Chifu".

Nilimwacha akiwa anataka kuzungumza mengi na mimi. Nilipanda ngazi na kuingia ofisini kwa chifu.

"Anatusubiri, amesema nichukue ripoti yako", Maselina alisema.

Basi tulifungua mlango na kuingia ofisini kwa Chifu. Chifu alikuwa amekaa kitini mwake akivuta mtemba kama kawaida yake.

"Shikamoo Chifu".

"Marahaba, ketini chini".

"Asante...

Maselina alichukua kitabu chake cha hatimkato na kukaa tayari kuandika mazungumzo yetu".

"Ehee, nieleze kwa kirefu mambo ambayo umeishafanya. Maana huko makamo makuu ya Polisi kuna kelele, mauaji ya ajabu yanatokea mjini hapa kwa mara ya kwanza mpaka wameshindwa mahali pa kuanzia upelelezi. Nilipopata ripoti yao juu ya mauaji haya, nilihisi hii ni kazi ya Namba Moja. Kwa hiyo naomba maelezo kamili ili nami niweze kuieleza serikali maendeleo yoyote juu ya jambo hili maana kuna wasiwasi mkubwa. Jumuia ya Ulimwengu inaikera serikali kwa kutaka kujua ukweli wa jambo hili, na wakati huo huo maadui zetu wanaendelea kutupaka matope bila kupata ukweli wa jambo hili".

Nilichukua muda huu kumweleza yote tangu nilipotoka ofisini mwake; kwenda kwetu bandarini na ofisi ya Kamati ya Ukombozi, barua niliyoikuta mlangoni kwangu; mapambano dhidi ya waliomteka nyara Sherriff na mwisho walioniteka nyara. Nilimweleza kila kitu kwa ufasaha bila kuacha tukio hata moja. Huenda jambo nililoacha ni juu ya tuliyofanya nyumbani kwangu na Veronika ambayo ni siri yetu hata nyinyi sitaki mjue.


"Kwa kutokana na maelezo ya mtu wa kikundi hiki kinachojiita 'Wanamapinnduzi wapinga mapinduzi' mimi naamini hawa watu ni VIBARAKA wa serikali ya makaburu ambao wanataka kupiga vita harakati za ukombozi dhidi ya serikali hizi dhalimu. Na mtu huyu niliyezungumza nae nina imani ni mtanzania kutokana na sura yake na sauti yake ingawaje alijitahidi sana kunidanganya kwa sauti.

Mimi ninavyofikiri kuna chama kimojawapo katika vyama vinavyopigania uhuru, ambacho makaburu wamekidanganya kuwa kikiweza kupiga vita harakati za mapambano ya silaha dhidi ya serikali ya Afrika Kusini itakipa mwanya chama hicho katika serikali ya makubaliano.

"Kwa hiyo chama hiki kimekubali kuwa kibaraka wa Afrika Kusini na kuanza vita dhidi ya vyama vingine vinavyoendeleza mapambano ya silaha. Kwa vile isingekuwa rahisi chama hiki kufanya mapambano bila msaada. Serikali ya makaburu lazima inakipa misaada ya kila hali, yaani wagtu, silaha na fedha. Kwa hiyo Chifu, ni imani yangu kuwa silaha hizi hazikibwa na watu wengine ila majasusi wa makaburu ili kutimiza lengo lao hilo'.

Chifu alikuwa ananiangalia kwa makini sana kisha akatingisha kichwa.

"Nimekuelewa vizuri sana Namba Moja. Hata unavyofikiri mimi naona ni sawa. Lakini tatizo letu liko pale pale; watu hawa wamejipenyezaje nchini humu na sasa silaha hizo ziko wapi?. Maana silaha hizo ni za kisasa kabisa. Hatua uliyofikia kwa siku moja inaridhisha, tafadhali kazana zaidi katika masaa ishirini na manne yajayo tuwe na fununu zaidi.

"Hapa tuna vyama viwili, PLF na SANP na vyama hivi ndivyo vinaendesha mapambano ya silaha huko Afrika Kusini. Kwa hiyo tuna chama kimoja ambacho kiko nje ya nchi hii; ama kiko Afrika ya Kusini ama katika nchi jirani na ndicho kimejipenyeza kuvipiga vita hivi vyama viwili".

"Hata mimi nafiri hivyo. Kwani kuna vyama vingapi vinavyopigana na serikali ya Afrika Kusini?".

"Viko vingi, kati ya hivyo vitatu viko Afrika Kusini na vitano viko nchi ya nje, kwa hiyo jumla ni vinane".

"Hili ndilo tatizo la vyama vingi. kingekuwa chama kimoja yote haya yasingetokea", nilisema kwa huzuni.

"Siasa kijana, wanasiasa ndio wanaleta taabu ulimwenguni; ndio wanayumbisha vichwa vyetu. Kila mtu na siasa yake na imani yake, na kuna wengine hawana cha siasa wala cha nini; nia yao kutaka ukubwa ili wale", alijibu Chifu kwa uchungu mkubwa.
"Sawa, sisi tunaendelea na upelelezi wetu na ushauri wako nitauweka manani".

"Asante sana Namba Moja".

"Polisi wamefikia wapi?".

"Polisi hawajafika popote. Sasa ndio wamechanganyikiwa zaidi baada ya mauaji haya ya usiku. Hivyo mimi nakutegemea wewe, maana umefanya maendeleo mazuri".

Nilisimama nikampigia kope Maselina nae akaminya midomo kuzuia tabasamu alilotaka kunipa. Chifu alinifungulia mlango na kuniambia. "Nakutakia mafanikio katika kazi hii kijana".

"Asante Chifu", nilijibu kisha akafungua mlango.

"Kavae upesi twende zetu Komredi", nilimwambia Sherriff aliyetaka kubadilisha nguo.

"Dakika tano tu", alijibu kisha akaenda haraka haraka.

Ilikuwa saa tano tulipofika New Afrika baada ya kumchukua Sherriff kutoka kwa daktari akiwa anajisikia vizuri kabisa. Veronika ndiye nilikuwa nimewahi kumchukua kabla ya Sherriff.

"Kavae upesi, twende zetu Komredi", nilimwambia Sherriff aliyetaka.

"Dakika tano tu", alijibu kisha akaenda haraka haraka.

Ilikuwa saa tano na dakika kumi na tano tulipoondoka kuelekea Ofisi za PLF. Njiani tulimweleza yote yaliyokuwa yametupata jioni ile tukibakiza tu ile habari ya kwenda kwetu pamoja kulala nyumbani kwangu.

Ofisi za PLF zilikuwa mtaa wa Makunganya karibu na Achells Limited hivyo haikutuchukua muda kufika pale kutokea New Afrika.Tulitokea barabara ya Azikiwe, tukaingia mtaa wa Independence pale kwenye mzunguko wa sanamu ya Askari halafu tukakata kulia pale kwenye taa za usalama barabarani za mtaa wa Independence na Postway, na kuingia Postway. Tukatelemka kidogo mpaka kwenye mtaa wa makunganya moja kwa moja kwenye ofisi za PLF. Tuliegesha gari pale pale mbele ya ofisi tukatelemka na kuingia mapokezi. tulimkuta kijana mmoja akiwa mapokezi.

"Habari zako ndugu", nilimsalimu.

"Salama, sijui niwasaidie nini?".

"Tunaomba kumwona ndugu Cecil Chimalamo".

"Mna miadi naye?'.

"Hapana, lakini ukimweleza kuwa kuna waandishi wa habari toka gazeti la Afrika natumaini anaweza kutuona".

"Subirini hapa kwenye viti".

Tulikaa kwenye makochi mazuri sana. Cecil Chimalamo nilikuwa ninamfahamu kwa sura na vile vile mambo yake kwani nilikuwa nimeshasoma faili lake mara nyingi ofisini. Kwa kifupi wanasiasa wengi walimpenda kwa sababu ya imani zake za kisiasa ambazo mara nyingi zilikuwa na msimamo. Alitambulikana kama kiongozi mmojawapo mashuhuri mpinga ubaguzi na mpenda serikali ya wengi katika Afrika ya Kusini, makaburu walimchukia sana.

Punde yule kijana alirudi akayakatisha mawazo yangu juu ya Chimalamo.

"Mnaweza kumwona chumba namba tatu".

"Asante', nilishukuru kwa niaba ya wenzangu.

Tulikwenda moja kwa moja mpaka chumba namba tatu tukabisha hodi.

"Karibu".
Nilifungua mlango tukaingia ndani tukajikuta katika ofisi.

"Karibuni", alitukaribisha huku akisimama.

"Asante".

"Nyinyi ndio mmetoka kwenye ofisi za gazeti la Afrika".

"Ndio".

"Twendeni mzee anawasubiri".

Alifungua mlango, tukaingia ndani na kumkuta ndugu Chimalamo amekaa anavuta sigara. Alipotuona alisimama.

"Karibuni, ketini chini".

Kabla hatujakaa nilichukua mwanya huu kujijulisha mimi pamoja na wenzangu kwake.

"Mimi naitwa Willy Gamba na ni Meneja Mkuu wa Kampuni iitwayo Afrika Internation Agencies (AIA), na hawa ni waandishi wa gazeti la Afrika. Huyu anaitwa Veronika Amadu na huyu ni Ahmed Sherriff. Wote ni wananchi wa Sierra Leone", tulishikana mikono na kusabahiana halafu tukaketi chini.

"Imekuwaje wewe uwe pamoja nao?", aliuliza.

"Kampuni yangu ndiyo wakala wa gazeti la Afrika hapa Tanzania kwa hivyo haja zao zote naziwakilisha mimi.

"Aisii, nafikiri tumeshaonana mara nyingi. Wewe si mgeni kabisa kwangu ", aliniambia na kuniangalia kwa macho ya kudadisi.

"Bila shaka tumeonana mara nyingi hasa katika tafrija za vyama hivi ingawaje hatujawahi kujulishwa moja kwa moja".

"Ehe gazeti la Afrika linataka nini?", Nilishangaa sana maana hata hakuuliza vitambulisho. Mara moja nikajua mtu huyu aliweza kuwasoma watu na kujua ni watu wa namna gani. Alikuwa mtu mwenye busara nami nikaondokea kumpenda.

"Sisi tumekuja hapa mjini baada ya kupata habari za tukio lililokikabiri chama chako na serikali ya Tanzania kwa ujumla. Jumuia ya Ulimwengu mpaka sasa imegawanyika katika pande mbili. Moja inalaumu Serikali ya Tanzania kuwa ndiyo inahusika na wizi wa silaha hizi ambazo ni za kisasa kabisa, upande wa pili unaamini kuwa hizi ni njama za mabeberu zinazopiga vita harakati za ukombozi wa Afrika Kusini. Kwa hiyo gazeti la Afrika likiwa kila siku linafuatilia kwa makini harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika na kuweza kusaidia inapowezekana, linahitaji hasa ukweli wa tukio hili. Hii ndio sababu tuko hapa. Tumeshawaona wakuu wengine katika OAU na katika Serikali ya Tanzania na tumeona hatuwezi kufika mbali bila kujua mawazo yako wewe ambaye ndiye hasa uliyehusika na mali iliyopotea", Sherriff alieleza kwa kinagaubaga.

"Kwa hiyo mnataka kujua mimi niko upande gani katika mawazo hayo mawili ya Jumuia ya Ulimwengu?".

"Hilo ndilo swali letu la kwanza", Sherriff alijibu.

"Mimi nawaunga mkono wanaoamini kuwa hizi ni njama za mabeberu. Wale wanaosema Tanzania inahusika wanajaribu kuongeza petrol kwenye moto huku wakijua kuwa Tanzania ni nchi pekee katika Afrika ambayo haiwezi kufanya jambo hili. Nakuhakikishia kwamba tangu nikae hapa nina miaka sita na sijaona Serikali ya kimapinduzi kama hii. La hasha, Tanzania haiwezi kabisa kufanya jambo hilo ila hizo ni mbinu za mabeberu za kutugonganisha sisi na wenyeji wetu ili mambo yaharibike kabisa. Mimi sitakubali washenzi hao watugonganishe. nafikiri umenielewa.

"Nimekuelewa sana. Sasa unafikiri silaha hizi zimepotea poteaje?. Hapa nataka mawazo yako binafsi".

"Hata mimi sijui. Ni njama ya hali ya juu iliyofanyika, hivyo nimeachia shauri hilo Serikali ya Tanzania ambayo imeniahidi itafanya juu chini kufichua njama hizi".

"Na isipowezekana?", Veronika aliuliza.

"Tutajua la kufanya wakati huo.

"Ilibainikaje kama wewe umekwenda Urusi kutafuta silaha za kisasa na hali naamini jambo hili lilifanywa kwa siri?", Sherriff aliuliza.

"Siku hizi hakuna kitu cha siri. Nafikiri hata kabla sijaondoka hapa Dar es Salaam kwenda Moscow ilikuwa imeshajulikana nini nafuata. Ulimwengu huu wa teknolojia hakuna kitu cha siri. Hata mkutano uliofanyika huko camp Davis Marekani, kati ya Marais wa Israel, Misri na Marekani na kuweka hali ya uficho wa hali ya juu, bado watu walijua kabla mazungumzo hayo ya kisiri ya hali ya pekee hayajatangazwa rasmi. ili kujibu swali lako hata sisi hatukutegemea tutajulikana.

"Watu wanafikiri kuwa, silaha hizo zimefanyiwa njama za kuibiwa kwa sababu ni silaha za kisasa kabisa na za hali ya juu. Ndio sababu watu wanasema Tanzania isingeweza kuziona zinakwenda hivi hivi. Sasa swali langu ni kwamba kwa nini uliamua kuomba silaha za kisasa za jinsi hii wakati vita havijafikia hali ya juu sana kuhitaji silaha za namna hiyo.

"Ahaa, swali lako zuri sana. Ili mwelewe kwa nini nilichukua hatua hiyo ni lazima niwape maelezo kamili, juu ya hali ya silaha alizonazo adui tunayepigana naye", alinyamaza kidogo akaegemeza mikono yake mezani.

"Maana mtu hawezi kupigana kwa rungu dhidi ya mtu mwenye bunduki. Kwa hiyo hamtajali naona nikiwaeleza kwa kirefu jinsi wapinzani wetu walivyojidhatiti kijeshi na ndipo tu mnaweza kuona kwa nini niliagiza silaha za kisasa".

"Sisi tutafurahi sana kupata fursa ya kusikia maelezo hayo", nilijibu kwa niaba ya wenzangu.

"Katika miaka 15 iliyopita", alieleza Chimalamo. "Makampuni ya kimataifa yamezidisha rasilimali zao ili kuimalisha uchumi wa Afrika Kusini. Makampuni makubwa ya Marekani na Ujerumani Magharibi yamepanua rasilimali zao katika sehemu muhimu za utawala wa Makaburu. Na makampuni haya yana ushirikiano mzuri sana na utawala wa Makaburu.

"Miaka michache iliyopita mabenki ya kigeni yameikopesha afrika Kusini mamilioni ya fedha ili kuwezesha kukabili migogoro ya kiuchumi iliyosababishwa na kulegalega kwa uchumi wa nchi za magharibi na kuendelea kukua kwa mapambano ya wazalendo wanaokandamizwa na utawala wa Makaburu.

"Mabenki ya kigeni yametoa mtaji mkubwa kwa utawala wa Makaburu kwa mahitaji ya fedha kwa ajili ya mambo ya kijeshi na kiuchumi, katika miaka michache iliyopita deni la kigeni la Afrika Kusini limeongezeka haraka kufidia gharama za mafuta yake, kupanua ununuzi wa silaha na gharama za mipango ya kuuwezesha utawala huo dhalimu ujitegemee. Kwa taarifa yenu mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 1976 utawala wa Makaburu ulikuwa na deni lipatalo Shs.72 bilion, lakini idadi inaweza kuwa kubwa kuzidi hapo maana mikopo kwa Afrika Kusini ni siri. Sijui mnanielewa?".
"Tunakuelewa sana", tulijibu kwa pamoja, huku Veronika akiwa anaandika maelezo hayo.

"Kuna ukweli unaoonysha jinsi biashara ya makampuni ya kigeni na rasilimali zao zilivyosaidia kuimarisha viwanda vya kijeshi vya Afrika Kusini hata kuuwezesha utawala wa Makaburu kuwa na kiburi na kupuuza maoni ya dunia na kuendelea kudumisha udhalimu wake na kuwakandamiza wananchi walio wengi wa Afrika Kusini.

Makampuni ya kigeni yamejihusisha moja kwa moja katika kuimarisha kijeshi Afrika Kusini. Kumbukumbu za kampuni moja inayoshughulika na utengenezaji wa silaha katika nchi zinazoendelea zinaonyesha kuwa makampuni ya kigeni yametoa liseni kwa makampuni ya Afrika Kusini kutengeneza zana za kijeshi za aina mbali mbali, pamoja na ndege za kijeshi, mabomu, risasi na bunduki. Vile vile kuna makampuni yanayotengeneza vipuri na vifaa vingine kwa madhumuni ya kijeshi. Shirika la Baruti na madawa la Afrika Kusini 'AECI' linatajwa kuwa linamiliki viwanda vitatu vinavyotengeneza silaha na linashirikiana na kampuni moja ya viwanda vya madawa ya Uingereza. "Imperial Chemical Industries", Kampuni hiyo ya Uingereza., imetoa utaalamu na vifaa vinavyotumiwa na Shirika la AECI la Afrika Kusini. Na wakati huo huo kampuni ya Darman Long ya Afrika Kusini iliyounda manowari moja yenye uzito wa tani 220 inashirikiana na Shirika la vyuma linalomilikiwa na serikali ya Uingereza katika shughuli za utengenezaji silaha".

Alinyamaza kidogo, akachukua sigara akaiwasha kisha akavuta mara tatu hivi halafu akaendelea.

"Kutokana na misaada hii toka nchi za Magharibi, Afrika Kusini imejiimarisha sana kijeshi. Utaona kuwa miaka ya sitini, matumizi ya kijeshi ya Afrika Kusini yameongezeka mara sita kutoka Shg 520 milioni hadi mwaka 1977/78 matumizi ya kijeshi yalikuwa yameongezeka tena na kufikia kiasi cha Shg 16,450/- milioni kwa mwaka. Nimetoa maelezo hayo pamoja na tarakimu ili kuwaonyesha kimsingi kuwa Afrika Kusini ina uwezo kifedha kutengeneza au kununua silaha za kisasa kabisa.

Alitua tena ili kuvuta sigara yake kisha akaendelea huku sisi tukimsikiliza kwa makini kama wanafunzi wanavyomsikiliza mwalimu katika somo wanalolipenda.

"Vijana lazima mtu ujue nguvu za adui yako kabla hujamkabili, la sivyo, utakuwa unafanya mapambano yasiyo ya kimsingi. Ili kuwapa ukweli hasa uliopo, jeshi la Afrika Kusini limekuwa likitumia zana za kisasa zilizoko duniani tangu mwaka 1970. Matumizi ya kijeshi kwa ajili ya kununulia silaha na vifaa maalumu vya kisasa vya kijeshi badala ya vya zamani yaliongezeka kwa asilimia 32 mwaka 1971 kufikia asilimia 53 mwaka 1973. Kati ya mwaka 1970 na 1979 Shg 2,240 milioni zilitumika kwa mambo ya ndege za kijeshi, shs 1,000/- milioni kwa ajili ya kununua radio, mitambo ya kutazama ndege angani (radar) na vifaa vingine vya kisasa. Kama nilivyokwisha kuwaeleza hapo awali, wakati huo huo utawala wa Afrika Kusini umekuwa ukichukua hatua kuimarisha utengenezaji wa zana humo humo nchini kadiri vipuli na vifaa vya mahitaji yake ya kijeshi yanavyozidi kuongenzeka.

"Kwa mjibu wa toleo moja la kijeshi la Marekani, tangu tangu mapema mwaka 1971 makaburu walikuwa wanaweza kutengeneza mabumu na baruti kiasi cha kujitosheleza na wanaweza kuuza nchi za nje. Juu ya risasi Afrika Kusini inatengeneza aina 100 za risasi. Kwa bunduki inajitosheleza kabisa. Kwa silaha za jeshi la nchi kavu, ama imejitosheleza ama imefikia hatua za utoaji, na itajitosheleza hivi karibuni kwa zana za jeshi la maji na sasa inatoa zana zote za moto inazohitaji. Bunduki za kisasa kama vile Rifle na Machine-gun vile vile zinatengenezwa. Hivi utengenezaji wa mizinga unaanza, na kuna huduma ya kuweza kutengeneza karibu kila aina ya magari ya kijeshi. Radio za ndege, vifaa vya kutegulia mabomu na vifaa vingine vya kisasa vya kijeshi vinabuniwa na kutengenezwa huko huko Afrika Kusini.

Alinyamaza na kuwasha sigara nyingine na kwa nguvu zile zile akaendelea kueleza.

"Hivi karibuni ilidokezwa kuwa Afrika Kusini inaunda aina fulani za bunduki, mabomu ya kudondoshwa na ndege yenye uzito wa kufikia ratili 1,000 kila moja na inaendelea na utengenezaji wa makombora ya kuangusha ndege. Mabomu hayo inasemekana yalifanyiwa majaribio mwezi Septemba 1977 kwa kutumia ndege za aina ya 'Mirage'. ndege hizi za mirage zilianza kuundwa huko Afrika Kusini chini ya liseni ya kampuni ya ufaransa ya Sessoult mnamo mwaka 1974. Kama hatua ya mwanzo. Afrika Kusini ilinunua vipande 50 vya ndege za aina hiyo na kuunda yenyewe ndege za mirage".

"Wakati huo vile vile ilikuwa tayari imeanza kuunda ndege za kijeshi aina ya Impala za muundo wa Italia-Armachi MB-326, magari ya kijeshi aina nyingi ya silaha ndogo ndogo pamoja na bunduki za aina ya rifle muundo wa Ubelgiji. Na kwa mjibu wa Waziri wa Uliniz wa Makaburu. Afrika Kusini ilitegemewa ianze kutengeneza vifaru vyake. Vile vile Afrika Kusini inasemekana imeanza kuendeleza utengenezaji wa mizinga ya kutungulia ndege aina ya CAC-TUS, ikisaidiwa na kampuni moja ya Ufaransa".

Alipofika hapa aliinua simu na kumwamru mwandishi wake mahsusi atuletee vinywaji baridi na sambusa kisha akaendelea.

"Naona nitawachosha lakini kwa sababu nyie wenyewe mmeuliza mimi nitawapa hali halisi ilivyo na mkiwa kama waandishi wa habari ni vizuri kujua hali ya kijeshi ya huyu adui wetu mkubwa katika Afrika. Kwa kutumia gazeti lenu mnaweza kujulisha jumuia ya ulimwengu ukweli wa nguvu za adui yetu huyu zilivyo, hivyo msitahimili karibu nitamaliza.

Mwandishi wake alileta vinywaji barudi na sambusa.

"Habari unazotueleza ni za kusisimua mno kwani kwetu sisi wengine ni habari mpya, hivyo hata ukiendelea mpaka usiku tutakuwa tayari kabisa kukusikiliza", nilimhakikishia.

"Kama hivyo basi nitaendelea. Magari ni muhimu sana katika mambo ya kijeshi. Kuna makampuni kadha wa kadha ya kigeni ambayo yamekuwa yakiisaidia Afrika Kusini kijeshi katika mambo ya magari. Makampuni hayo ni pamoja na kampuni ya Marekani ya General MOtors (GM), kampuni kubwa duniani inayotoa magari kwa wingi baada ya Vita Kuu ya kwanza. Hivi sasa ina mtambo wa kuunganisha na kuunda magari huko Port Elizabeth, na mtambo wa kutengeneza injini za magari nje kidogo ya mji huo.

"Kampuni nyingine ya magari ni ile ya Ujerumani inayotengeneza magari ya aina ya 'Benz'. Magari ya kijeshi ya aina hii ndiyo yanatumiwa sana na majeshi ya Afrika Kusini. Msemaji mmoja wa kampuni ya magari ya Benz na BMW, alijigamba hivi karibuni kwamba kampuni yake inatengeneza magari hayo Ujerumani kwenyewe na Afrika Kusini na inakusudia kutumia Afrika Kusini kama kituo cha kuuzia magari hayo kwa nchi za nje zilizoko Kusini kwa Ikweta. Hii inaonyesha dhahiri kuwa Afrika Kusini inayo magari haya zaidi ya mahitaji yake ya kijeshi".

Alinyamaza tena akachukua glasi yake iliyojaa Coca-cola akainywa kwa mara moja kisha akainua macho yake na sura yake ikageuka kuwa nzito kisha akaendelea.

"Na mwisho napenda kuwaeleza jambo la mwisho lakini muhimu si kwa sisi wapigania uhuru tu bali kwa Afrika nzima. Katika mwaka 1974 Shirika la Nyuklia la Marekani lililoko Oak Ridge lilipeleka kilo 45 za madini ya 'Uranium' kwa mtambo wa utafiti wa nyuklia uliopo Palandaba huko Afrika Kusini baada ya Tume ya Nyuklia, chombo pekee cha Marekani kinachotoa liseni za usafirishaji nje vifaa vya nyuklia kukubaliana na Afrika Kusini kwamba haitaruhusu madini hayo yapelekwe pengine au kutumiwa vinginevyo. Marekani vile vile mwaka 1975 na 1976 iliipa Afrika Kusini madini hayo yanayotumiwa kutengeneza zana za nyuklia na kuahidi kuuza zaidi madini hayo kwa mtambo wa pamoja na nguvu za nyuklia wa Marekani na Ufarasa unaotazamiwa kujengwa Afrika Kusini mwaka 1984. Kwa jumla Marekani imeiuzia au imeahidi kuiuzia Afrika Kusini ratili 300 za madini hayo kwa ajili ya mtambo wa utafiti wa nyuklia uliopo Palandaba. Kwa taarifa yenu ratili 300 za Uranium zinawza kutengeneza mabomu 15 ya Atomiki".

Kila mmoja alipiga mluzi wa mshangao.
"Nafikiri ndugu Willy nimejibu swali lako kwa kirefu, kwa hiyo utaona sisi wapigania uhuru hatuna budi kuomba silaha za kisasa zinazoweza kukabili nguvu hizi kubwa ya kijeshi za adui yetu. Kwa hiyo tukio hili lililotokea linaonyesha dhahiri kuwa hawa makaburu wameona hatari inayowajia hivyo kuiba silaha hizi ni mbinu moja ya kujihami. Na mimi nimeapa sitarudi nyuma nitaondoka tena karibuni kwenda kutafuta silaha za kisasa na kali toka nchi rafiki ambazo naamini zitaamini kuwa tukio hili ni njama za mabeberu. Hivyo njama zao zinazidisha tu moto katika wapigania uhuru na ndugu zao wanaowasaidia. Huu si mwisho wa mapambano. Ila ni matayarisho tu ya mapambano - historia itanihukumu. Mna swali zaidi?".

Tuliangalia na kukawa hakuna mtu mwenye swali kwani risala yake ilituchoma mioyoni kama miali ya moto wa umeme.

"Asante, tumetosheka", nilijibu kwa niaba ya wenzangu.

"Oke mnakaribishwa tena siku yoyote kwani katika kuzungumza nanyi ndipo tunapoweza kujua hali halisi ya Kusini mwa Afrika. Asante sana vijana wa Afrika kuja kunitembelea". Alitupa mkono wa kuagana.

"Asante sana", tulijibu na kuondoka ofisini mwake kimya kimya.

Tulipofika kwenye gari langu niliona ni saa saba u-nusu, kweli tulikuwa tumekaa sana ndani. Tuliingia ndani ya gari.

"Sasa twende tukaonane na Ray Sikazwe. Rais wa Chama za SANP

Ofisi za SANP zilikuwa barabara ya Umoja wa Mataifa baada ya kuvuka barabara inayoingia Hospitali ya Muhimbili. Hivyo niliendesha moja kwa moja na kuingia barabara ya Morogoro kutokea mtaa wa Makunganya. Tulipofika kwenye taa za usalama barabara za Jangwani, nilikata kulia na kuingia barabara ya Umoja wa Mataifa. Nilisimamisha gari karibu na mlango wa ofisi kwani kwa upande mwingine wa barabara kuna gereji na magari yalikuwa yamejaa kibao.

Tuliingia mapokezi na kumkuta binti mmoja anajipaka poda usoni. Alipotuona akaweka mkebe wa poda kando, alijifuta vizuri usoni halafu akatutolea tabasamu.

"Karibuni".

"Asante. Hujambo Binti?".

"Mimi sijambo, sijui niwasaidie nini?".

"Tunaomba kuonana na Ndugu Sikazwe.

"Mna miadi naye?".

"Hapana".

"Basi hawezi kuwaona, ana kazi nyingi sana. Huenda mnaweza kumwona ndugu Amos Shumka ambaye naye ni ofisa katika ofisi hii".

"Wewe ni Mtanzania?".

"Ndio".

"Basi dada sisi hatutaki kumwona mtu mwingine ila ndugu Sikazwe".

"Basi kaka yangu, ndio huwezi kumwona leo. Amesema hawezi kumwona mtu yeyote hata awe nani kama hana miadi naye. Mimi ninatii amri ya wakubwa wangu kwa hiyo siwezi kufanya vinginevyo".

"Jaribu kumpigia simu umwambie sisi tunataka kumwona tunatoka gazeti la Afrika, mwache yeye aamue".

"Hata kama mnatoka katika gazeti la dunia, siwezi", alichukua rangi ya midomo na kuanza kujipaka.

"Naona tumenoa", alisema Veronika.

"Basi, tutajipeleka wenyewe, twendeni", niliwaambia wenzangu.

Yule msichana alisimama na kututangulia haraka haraka na kuelekea kwenye ofisi moja huku uso wake umejaa hasira. Na sisi tukamfuata mbio mbio nyuma. Alipofungua mlango wa ofisi hiyo tu na sisi tukaingia.

Hawa watu nimewakatalia kumwona mzee lakini wamekuja kwa mabavu", alimweleza msichana mwingine aliyekuwa anapiga taipu. Kabla yule msichana hajajibu mimi nilipita mbele na kufungua mlango wa ofisi ya ndugu Sikazwe kwani bila huyu msichana kujua alikuwa ametuelekeza mwenyewe. Wasichana wote wawili walibaki wameshikwa na butwaa na kushika midomo yao. Mimi nilifungua mlango na wote watatu tukaingia ndani. Tulimkuta Ndugu Sikazwe anazungumza kwenye simu, na alipotuona tunaingia mara moja alikata simu na sura yake ikawa na hasira.

"Nani amewaruhusu kuingia ofisini mwangu kwa kikuku namna hii?".

"Samahani ndugu Sikazwe. Sisi tunatoka kwenye ofisi za gazeti la Afrika na tumekuja kukuona kwa jambo la maana sana kuhusu wewe na Afrika nzima. Sasa tulipofika hapa ofisini kwako mzee, msichana wa mapokezi akatukatalia tusikuone. Kwa sababu sisi tuna uhakika kuwa ungeturuhusu tuonane nawe, tumeona hatuna budi kufanya jambo lililo la busara, ambalo ni kujileta sisi wenyewe tukiwa na imani kubwa kuwa utatuona. Naamini umeelewa kwa nini tumechukua hatua hii, na ukiwa kiongozi mmojawapo mwenye busara kati ya viongozi wa vyama vya wapigania uhuru wa Afrika Kusini tuna imani utatupokea kwa mikono miwili. Jambo lililotuleta si jambo la kitoto", nilimweleza kwa utaratibu sana.

Ghafla uso wake ukabadilika. Tabasamu kubwa likaonekana usoni mwake naye akasimama.
"Samahani sana ndugu zangu katika jina la Afrika huru. naamini mtawasamehe hao wasichana pamoja na mimi, kwani ilibidi kutoa amri hiyo kwa sababu sasa hivi nashughulikia tukio ambalo limetokea hivi karibuni ambalo limevuruga vichwa vyetu. Msiwe na wasiwasi jioneni kama halikutokea jambo la kuwaudhi. Karibuni tuendelee na shughuli zilizowaleta".

Baada ya maelezo haya tulipeana mikono tukajulishana kisha tukaketi chini tayari kwa mazungumzo.

"Nafikiri ndugu Gamba tumewahi kuonana?", aliuliza.

"Ndio tumewahi kuonana kwenye tafrija nyingi".

"Umesema kampuni yako ndio wakala wa gazeti la Afrika hapa Tanzania?".

"Ndio".

"Aisee, haya mimi niko tayari tuendelee na mazungumzo yaliyowaleta".

Veronika alikohoa kuliweka koo lake vizuri kabla hajaanza kusema. Alipokuwa tayari alichukua uwanja.

"Gazeti la Afrika ni gazeti ambalo limekuwa na litazidi kutetea mapambano ya Kusini mwa Afrika. Hivi majuzi tumesikia tukio lililotokea hapa mjini, ambalo sisi tumelichukua kama pigo kubwa sana kwenye harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika. Ndio sababu tuko hapa ili tuweze kuzungumza na viongozi wa Serikali ya Tanzania na Maraisi wa vyama vya wapigania Uhuru walioko hapa nchini hivyo tuweze kupata mwanga wa jambo hili. Kumekuwa na uvumi wa kutatanisha ulimwengu mzima juu ya tukio hili.

"Kuna mambo mawili yanazungumziwa. Jambo la kwanza ni kwamba tukio hili limetokana na njama za mabeberu za kutaka kuzima harakati za ukomboni Afrika Kusini na ndiyo sababu silaha hizi zimeibiwa. Wengine wanalaumu serikali ya Tanzania kuwa ndiyo iliyofanya njama hizi kwani silaha zilizokuwa zimekuja. Serikali yoyote hata iwe ya kimapinduzi namna gani ingeweza kupata kishawishi cha kuchukua silaha hizi kwa manufaa yake. Sijui wewe una mawazo gani juu ya jambo hili", Veronika aliuliza baada ya kutoa maelezo haya marefu.

"Kusema kweli mimi bado nimechanganyikiwa juu ya tukio hili. Mambo yote haya mawili nimeyasikia lakini bado mimi sijasikia uamuzi jambo lipi ni sawa. Kama mlivyonikuta hata mimi najaribu kuzungumza na maofisa mbali mbali wa serikali ya Tanzania na Ofisi ya ukombozi ya OAU ili na mimi nipate msimamo wangu. Tukio hili si la kukimbilia kuamua".

"Kwa hiyo tuseme una wasiwasi kuwa huenda ikawa kweli Serikali ya Tanzania ikawa inahusika?", aliuliza Veronika huku macho yake yakimwuliza Sikazwe.

"Sikazwe alisita kidogo akajaribu kukwepa macho ya Veronika.

"Sina wasiwasi na Serikali ya Tanzania kuhusika na tukio hili, lakini ili niwe na uhakika vile vile ni lazima nichunguze upande huo vile vile. Msinielewe vibaya, mimi ni mtu ambaye mara kwa mara hupenda kuchunguza mambo na nipatapo ukweli nang'ang'ania kwenye ukweli. Sijui mumenielewa?".

"Mimi nimekuelewa kuwa utakuwa na uhakika tu kuwa Tanzania haijahusika utakapopata ukweli wa jambo lilivyo", Veronika alijibu.

Sikazwe alisita tena.

"Kitu kama hicho. Mnajua sisi wapigania Uhuru tuko katika hali ya kutatanisha sana. Kwa sababu serikali za nchi huru za Kiafrika unakuta moja inapendelea chama hiki nyingine chama kile maana sisi tuko vyama vingi. Hivyo ili kuamua jambo hili ni lazima uangalie mambo mengi", alijibu.

"Kama nimekuelewa vizuri unatupa tena hali ya tatu kuwa huenda si Tanzania wala mabeberu waliohusika katika njama hizi ila inaweza kuwa nchi mojawapo katika nchi huru za Kiafrika", nilisema.

"Nafikiri sasa umenipata".

Sisi tuliangaliana kwa mshangao kwani fikra hii ilikuwa haijaingia vichwani mwetu.

"Vizuri tumejua msimamo wako", nilijibu.

"Kwa hiyo ili niweze kuwapa msimamo wangu kamili mnipe muda ili niweze kutuliza mawazo yangu baada ya kuzungumza na watu fulani".

"Unamjua kijana mmmoja aitwae George Kiki", Sherriff aliuliza.

Sura ya Sikazwe ilionyesha mshituko ambao ni mtu kama mimi tu ambaye angeweza kuona.

"Ndio ninamkumbuka aliwahi kuja hapa ofisini kwangu akiwa mkimbizi kutoka Afrika Kusini baada ya matatizo ya Soweto. Na sisi huwa ni wajibu wetu kama chama cha wapigania uhuru kuwasaidia. Tokea siku hiyo mpaka leo sijapata kumwona tena. Je ana nini?".

"Amekutwa ameuawa nyumbani kwake", Sherriff alimjibu.

Sikazwe alionyesha hali ya mshangao.

"Nimesikitishwa sana; alionekana kijana mzuri".

Simu ililia Sikazwe akaichukua.

"Sikazwe hapa".
Akaisikiliza kwa muda halafu akajibu. "Sawa, nakuja sasa hivi".

Akakata simu.

ITAENDELEA

0 Reviews