Read more
Simulizi : Barua Kutoka Jela
Sehemu Ya Kwanza (1)
Ilikuwa ni Jumapili moja tulivu, majira ya asubuhi. Gereza la keko lilikuwa katika pilikapilika, kama ilivyo kawaida yake katika siku za mwisho wa wiki! Watu walikuwa wengi sana wanaandikisha majina yao, na majina ya ndugu na jamaa zao waliokwenda kuwatembelea katika Gereza lile. Karatasi zilizojaa majina zinapelekwa ndani Gerezani, ili kuitwa majina ya watu walioandikishwa na jamaa zao pale nje, iwe ni Mahabusu au Wafungwa. Nani lazima uandikishwe jina lako, jina la Mahabusu au Mfungwa uliemtembelea, sehemu unayotoka, na uhusiano uliopo baina yako na mtu uliemtembelea.
“Oyaa hapa watakaoingia ni wale watu waliokuja, na vitu vya kuwaletea ndugu na jamaa zenu, kama hujaja na chakula, au chochote, duka letu lile palee mkanunue”.
“pia sehemu yakuongelea na jamaa zenu ni ndogo, haitoshi kuingia watu wengi kwa wakati mmoja. Hivyo mtaingia watu kumikumi, kufuatana na namba za majina ya karatasi mlioandikishwa!”
Ilikuwa ni sauti ya askari magereza iliyokuwa inawafahamisha wale wageni waliokwenda katika Gereza la Keko Jijini Dar es salaam.
Upande mmoja wa eneo lile, alikuwa amesimama Dada mmoja mwembamba, mrefu wa wastani akiwa amembeba mtoto mdogo mgongoni wa takribani miaka mitatu au minne hivi. Mkononi mwake dada yule alikuwa amebeba kikapu,chenye vyombo ndani yake vilivyowekwa chakula, alikuwa muda mrefu amekosa furaha, sura yake ilitawaliwa na simanzi kubwa. Alikuwa amezama katika lindi la mawazo!
“Wee sikiliza hiyoo, haina kurudia hii, naita majina ya ndugu zenu walioitika majina yao huko ndani,kama hukusikia jina la ndugu au jamaa yako katika karatasi hii namba moja, na wewe umeandikisha katika karatasi hii na zingine zitakazofata. Basi ujue ndugu yako hayupo katika Gereza letu.” Ilikuwa sauti ya askari Magereza iliyokuwa katika lafudhi ya luhga ya watu wa Jela, ikiwataka wageni kuwa makini katika kusikiliza. Kisha akaanza kuita majina yale aliyokuwa nayo mkononi mwake, moja baada ya jingine, hadi jina la kumi akamaliza kwa kulitaja jina la MWADUGA DINGO.
“Haya aliesikia jina la ndugu yake anifate, ili akaongee na ndugu yake, na kama hukusikia jina la ndugu yako, basi huenda akawa katika Gereza la Segerea au Ukonga, nendeni huko mtawapata.”
Alimaliza kusoma majina na kutoa ufafanuzi askari yule, kisha akaongoza mbele huku akifatwa na kundi la watu kumi nyuma yake, kwenda kuwaona ndugu na jamaa zao, waliopo Mahabusu, na waliofungwa katika Gereza lile la Keko.
“Wee Dada unaitwa nani na kwa nini umekuja na mtoto mdogo huku? haturuhusu watoto wadogo kuletwa magerezani, kwani mtakuja kutuletea vilio tu huku!” Ilikuwa ni sauti ya askari magereza aliekuwa akimuhoji yule Dada aliekuwa amembeba mtoto mgongoni, ambae muda mwingi alikuwa katika simanzi.
“Mimi naitwa Eshe Muhidini, Mume wangu Mwaduga Dingo yupo humu Gerezani, nami sina mtu wa kumuachia mwanangu, ingawa pia nilikuwa sitambui kama watoto hawaruhusiwi kuja nao huku!”
“Haya leo nakuruhusu uongee na mumeo, ila siku nyingine usije na mtoto Gerezani, sawa?”
Eshe aliitikia kwa kuinua kichwa lakini hakufungua mdomo wake kumjibu yule askari, akapiga hatua moja kubwa kuingia ndani ya mlango mkubwa wa magereza, na akaonana uso kwa uso na mumewe Mwaduga Dingo, aliekuwa upande wa ndani, na yeye Eshe akiwa upande mwingine, wakitenganishwa na bomba za chuma, zilizojengwa maalum, bila shaka kwa ndugu jamaa kuonana na ndugu zao waliokuwa ndani katika gereza lile, kama Mahabusu au Wafungwa.
“Tunatoa dakika mbilimbili kuongea na kumkabidhi kitu au chakula ndugu yako uliekuja kumuona, kwani nje huko kuna kundi la watu wengi nao pia wanataka kuja kuwaona ndugu zao.”
“Pia kitu chochote unachotaka kumpa mahabusu au mfungwa, lazima umpe askari, akikague kwanza,kisha askari atamkabidhi muhusika.”
“Na ikiwa umeleta chakula, lazima uonje kwanza ndiyo tumpe mlengwa. Ila mliokuja kuwaona wafungwa, hao hawaruhusiwi kupewa chakula cha nyumbani, wala nguo za kiraia, hawa ni watu wetu washakubali, hivyo wanakula chakula cha jela hadi kifungo chao kitakapomalizika, sambamba na kuvaa sare za kifungwa. Isipokuwa maji, sabuni, mafuta, mswaki, dawa ya meno, na nyembe ruksa kuwapa.”
Ilikuwa sauti ya askari wa zamu, alikuwa akitoa taratibu za lazima katika sheria za Magereza.
Eshe alisogea karibu, na zile bomba, huku akibubujikwa na machozi, na kumwambia mumewe,
“Pole mume wangu, kuwa na subira mungu atakujaalia, utatoka tu ili tuje tumlee mtoto sote.”
“Asante mke wangu, nawe pia kuwa na subira, kwani mimi najua siku ya kuingia humu gerezani, sijui lini nitatoka.”
Mwaduga Dingo aliposema maneno hayo, akashindwa kujizuia akaanza kulia, kwani mwanae alikuwa anataka kutoka katika mgongo wa mama yake alipobebwa, akitaka kwenda kwa baba yake.
“Haya ndiyo maana sisi haturuhusu watoto kuingia nao humu ndani kwani yanamuumiza huyu aliyoko ndani, umeona sasa mama mtoto ee?!”
Yule askari magereza, alimkaripia Eshe Muhidini kwani sasa kulikuwa ni kilio kutoka kwake, kwa mwanae, na kwa baba mtoto.
Mwaduga alifuta machozi, akaingiza mkono mfukoni mwake mwa suruali, akatoa barua na kumkabidhi askari wa zamu aliekuwa makini katika kuangalia kila kinachotoka, na kuingia katika vile vitu walivyokuja navyo wageni, kuwaletea ndugu zao.
“Afande naomba hii barua umpe mke wangu, anipelekee maskani, akawape madereva wa taxi wenzangu.”
Mwaduga alinyoosha mkono wake wenye barua, akamkabidhi Yule afisa wa zamu, nae Yule askari aliipokea, akaifungua na kuisoma. Baada ya kujilidhisha kuwa ile barua haina madhara kwa usalama wa Gereza, Yule askari afisa wa zamu, alimuangalia Mwaduga usoni, na Mwaduga nae akamkazia macho Yule askari, kwa sekunde kadhaa. Kisha Yule askari, akamkabidhi ile barua mke wa Mwaduga.
Eshe aliipokea ile barua huku bado machozi yakimbubujika machoni mwake, midomo yake ikitetemeka na kugongana mithili ya mgonjwa mwenye homa kali.
“Haya muda wenu umekwisha, na wenzenu nao, wanataka kuingia.”
Yule askari wa zamu alitoa amri, ya watu kutoka nje, na Mwaguga aligeuka huku akibeba chakula, na vitu alivyoletewa na mkewe,akirudi ndani ya gereza, huku nyuma mkewe Eshe binti Muhidini, sasa akaangua kilio kwa sauti ya juu, na mwanae pia akimlilia baba yake, akawa analombokeza, katika huzuni iliyotawala katika familia yao, kwa ghafla!
Mwaduga akasimama huku nae akilia,akamwambia mkewe kwa sauti ya huzuni na unyonge.
“Nyamaza kulia, muangalie mtoto, pia hakikisha hiyo barua unawapelekea jamaa kijiweni, niombee dua mke wangu nita…………!”
Mwaduga alishindwa kumalizia kalima aliyoikusudia, kwani mkewe, Eshe alitolewa nje na mlango ukafungwa!
Eshe aliondoshwa pale baada ya muda uliowekwa wa watu wa awamu ya kwanza kumalizika, huku akiwa mnyonge na mwanae akiwa anamlilia baba yake, huku akiwa anataka kuchomoka mgongoni ili aende kwa baba yake, Eshe alimdhibiti mwanae huku na yeye machozi yakimtoka. Mwaduga alikuwa katika wakati mgumu sana, kumuona mtoto wake wa pekee anataabika namna ile.
Eshe alitoka nje ya eneo la magereza, huku akiwa analia kwa kwikwi. Akaivuta kanga yake akawa anaifutia machozi, akawa analia huku anatembea hadi nje ya eneo la Magereza. Mara akatokea Dada mmoja, akamfuata Eshe pale alipokuwa. Kwani sasa alikuwa ameegemea kiambaza cha nyumba moja, iliyozungushiwa mabati inayoendelea na ujenzi, na kumuuliza “kulikoni?!”
Eshe akamfahamisha kuhusu barua aliyopewa na mumewe ambaye ni mahabusu, akimtaka awapelekee madereva Taxi ili wamfatilie, kitu ambacho kinamliza Eshe na kuona kuwa hakitamsaidia mumewe kutoka. Kwani tokea mumewe apatwe na matatizo, hajamuona Dereva wa Taxi yoyote kuwa Karibu nae, isipokuwa wakitokea kukutana njiani kila mmoja hujitia anaguswa sana!
“Pia hatuna pesa yakuweka Wakili, hivyo mimi na mtoto wangu tunaishi katika mazingira magumu. Kwani hata wazazi wetu wapo mbali,wanaishi Tanga mpakani na Mombasa”.
Eshe alimwambia yule Dada msamalia.
Yule dada akamuhurumia sana Eshe na mwanae, na kumpa pole huku akifikiri, aliingiza mkono mfukoni na kutoa simu. Alibonyeza namba kadhaa na kuiweka sikioni.
“Wee usiniambie! yaani jumaapili yote hii upo kazini!?” Yule dada alizungumza na mtu aliekuwa anawasiliana nae.
“Sawa sasa naomba nisaidie jambo moja, kuna dada mmoja hapa ninae, ninamuelekeza aje kwako, tafadhali naomba umsaidie kadiri ya uwezo wako”.
Baada ya kusema hayo, yule dada akakata simu, Kisha akamuelekeza Eshe aende kwa mtu alietoka kuongea nae muda si mrefu, akampa na pesa kiasi cha shilingi elfu mbili, ili afanye nauli.
Eshe akamshukuru yule dada mwenye machozi mateke, na kuelekea sehemu aliyoelekezwa aende akiwa na barua yake mkononi.
Eshe akiwa na mwanae mgongoni, ambae sasa alikuwa amelala baada ya kilio cha kufa mtu! Alitembea hadi katika kituo kiitwacho TAMECO, akasubiri daladala zinazokwenda posta, na haikuchukua muda mrefu, ikaja gari inayofanya safari zake TANDIKA, POSTA akapanda.
*******
Eshe alikuwa yupo wizara ya mambo ya ndani ya nchi, pale maeneo ya Posta mpya. Akitazamana na Dada mmoja mwenye sifa zote za kuitwa mrembo. Kule uani mwa jengo lile, kwenye ofisi za mbao. usingeweza kabisa kuamini kuwa yule dada angeweza kuwa askari, kwa jinsi alivyopendeza. Namna alivyopangilia nguo zake, na zilivyo mkaa. Kifupi yule dada alikuwa ana damu ya nguo!
“Karibu dada Naitwa Inspekta Jamila, sijui nikusaidie nini?”
Eshe aliulizwa na yule mwenyeji wake aliemkusudia.
“Mimi Naitwa Eshe Bint Muhidini, amenielekeza dada mmoja aliekupigia simu muda si mrefu.” Eshe alijibu na kujitambulisha kwa mwenyeji wake.
“Ahaa, wewe ndiye aliekuelekeza Dokta Zahala? Upoje nae yule, kwani ni shoga yangu mkubwa yule, toka tukiwa Shuleni. Na ndiyo Daktari wangu.”
Eshe akamueleza mazingira aliyokutana nae yule dada, ambae sasa amemtambua kuwa ni Dokta Zahala.
Mwisho akamueleza kilichompeleka pale, na kumkabidhi ile barua.
Inspekta Jamila aliipokea na kuisoma. Ilikuwa ni barua ndefu, iliyoandikwa katika mtindo wa Shairi, ikiwa na kichwa kilichosomeka BARUA KUTOKA JELA. Ilikuwa ikisomeka hivi.
Naiandika barua, hapa nipo gerezani
Natuhumiwa kuua, eneo la mikocheni
Hakika ninaijua, sihusiki asilani.
Tuhuma ya jambo zito, kama hili maishani
Bora nipakate moto, niungue miguuni
Kuliko kuwa na joto, lisilokwisha moyoni
Mimi ni Taxi dereva, nikipaki magomeni
Akaja bwana Mzava, enda Sinza kijiweni
Kumbe baa linawiva, mimi kuwa hatiani.
Nilipokuwa narudi, barabara ya namnani
Nilimuona Masudi, tunaishi majirani
Nami sikuwa na budi, bali kupaki pembeni.
Wakaja watu watatu, wakaingia garini
Tunazo elfu tatu, tupeleke kwa Macheni
Wana begi na viatu, wameshika mikononi
.
Masudi nikamwambia, tutaongea nyumbani
Huku nikitia gia, kurudi barabarani
Pia nikifurahia, kurudishwa maskani.
Baa likaja timia, tulipofika mwishoni
Askari wa doria, walikuwa kwa Macheni
Jamaa walikimbia, wakawacha begi ndani.
Askari walinivamia, na bunduki mikononi
Nikiwa nimetulia, sijui nifanye nini
Nikapigwa pasi hatia, kila sehemu mwilini.
Kivumbi sasa sikia, ndani ya begi kuna nini
Namba za gari bandia, na “Sub mashine gani”
Bastola naishuhudia, na Risasi ishirini.
Kisha nikafungwa pingu, nikapelekwa kituoni
Akaja tajiri yangu, nikapata ahueni
Akapakiwa majungu, akaniona shetani.
Akataka gari yake, aitoe kituoni
Sikuwa na mana kwake, kanitelekeza ndani
Huyoo akaenda zake, namchungulia dirishani.
Habari zilienea, zikasambaa mjini
Jambazi lilozowea, limenaswa mtegoni
Walionitembelea, wengi hawakuamini.
Walikuja ndugu zangu, jamaa na majirani
Mke na mtoto wangu, machozi tele machoni
Baba angu baba angu, analia Marijani.
Uchungu nilionao, hausemeki mdomoni
Unamuwacha mwanao, kwa kuwa kizuizini
Kula na kuvaa yao, ishakuwa mtihani.
Polisi wakachunguza, kiasi siku sitini
Huku wakiniongoza, kuenda mahakamani
Kesi wakaigeuza, nikaletwa gerezani.
Robali ikawa Mada, mazito haya jamani
Bastola ile ya kimada, wa bosi Serikalini
Anaeitwa Hamida, kauwawa mikocheni.
Mimi naweza kunyongwa, hadi kufa kitanzini
Nataka wakili bingwa, pesa sina mifukoni
Nilipo nina magonjwa, kwa kupewa milo duni
Taxi dereva wenzangu, popote pale nchini
Nauaga ulimwengu, bado ninautamani
Someni Barua yangu, kisha nisaidieni.
Karatasi inajaa, ndugu zangu Buriani
Imenijaa fadhaa, na donge tele moyoni
Kuonyesha mashujaa, walau andamaneni.
Naomba wasamalia, mwanangu nileleeni
Atawalipa Jalia, hapahapa duniani
Mimi mola namwachia, walimwengu kwaherini.
Ilimaliza barua ile katika namna ya kuhuzunisha na kugusa moyo ulio hai.
-
Ilimaliza barua ile, huku Inspekta Jamila akiwa makini akamtazama Eshe huku akimuhurumia sana, akamwambia.
“Nimeisoma hii barua na imenigusa sana, kiasi kwamba kwanza itanibidi nimuone huyo Mumeo aliekutwa na mkasa mzito kama huu, kisha nipembue ukweli upo wapi? Ndiyo nitajua nawezaje kumsaidia.”
“Hivyo naomba niandikie majina yake kamili, na sehemu mnayoishi, namba ya nyumba na jina la mjumbe wa eneo hilo. Kisha wewe nenda uje unione siku ya Jumamosi, ili ujue nilipofikia”.
Eshe akafanya kama alivyoagizwa na kisha akaagana na Inspekta Jamila huku akimuachia na ile Barua kutoka jela, akaondoka akiwa na matumaini kiasi.
Inspekta Jamila baada ya kuagana na Eshe aliendelea kukaa mle ofisini mwake, huku akiwa na mawazo tele, kwani ile barua ilimgusa kiasi ilimkosesha raha kwa wakati ule. Aliifungua tena karatasi ya barua ile na akairudia upya kuisoma, hatimae akakata shauri.
Aliangalia saa yake ya mkononi na kuona kuwa ni saa sita adhuhuri, hivyo alifungia baadhi ya vitu katika droo za kabati lake la pale ofisini, na kutoka nje ya ofisi yake akiazimia kwenda katika gereza la keko!
*******
Mwaduga Dingo akiwa na Ispekta Jamila, pamoja na askari magereza wa kiume, walikuwa wamekaa katika chumba maalum, Mwaduga akichukuliwa maelezo na kutakiwa amsimulie kila kitu anachokumbuka hadi yeye kuwa mahala pale akiwa ni Mahabusu!
Mwaduga Dingo alianza kufikiri, na kuanza kumuhadithia. Inspekta Jamila Tangu akodiwe na Bwana Mzava hadi Sinza, kisha alivyokuwa anarudi barabara ya Namnani alipomuona Masudi na yeye kupaki pembeni.
Akamuhadithia walivyokuja watu watatu wakiwa wamebeba Begi na viatu mikononi, na kuingia Garini kwake huku wakimwambia bei na sehemu wanayokwenda, hadi yeye alipomuaga Masudi, na hata tukio lililotokea pale kwa macheni jamaa walipokimbia na kuacha Begi ndani ya gari yake!
Pia kipigo alichokipata na kufungwa pingu hadi kituoni! Kiasi maelezo yake hayakupishana hata kidogo na barua aliyoiandika, ambayo Inspekta Jamila anayo na ameipa jina la Barua kutoka jela.
Inspekta Jamila aliyaandika yale maelezo na kisha kumtupia swali Bwana Mwaduga.
“Ehe baada ya kupelekwa Kituo cha Polisi nini kilifuata?.”
Mwaduga akamueleza. “Niliteswa sana ili niwataje wale abiria wangu, ambao polisi wakati wote wanawaita wenzangu waliokimbia! Ilihali ya kuwa mimi siwatambui! Baadae walikuja watu wa Habari na kunichukua picha za video, na picha mnato.”
“Baadae Tajiri yangu ambae ndio mmiliki wa gari akaja pale kituoni. Maaskari walimwita chemba na kuzungumza nae! Bila ya shaka walimtisha au kumwambia kuwa mimi ni Jambazi! Kwani hakutaka kuniuliza kilichotokea, sikwambii kuniona. Aliondoka huku akiwa amelowa kwa maneno aliyopakiwa.”
“Walikuja jirani zangu, Mke na jamaa wengine ili wanichukulie Dhamana ya Polisi, lakini dhamana ilikataliwa! Yakitolewa maelezo kwamba, kuna wahalifu wenzangu ambao wamekimbia! Hivyo nikiwa nje kwa dhamana nitaharibu upelelezi, na sasa wanasema sitoweza kupata dhamana, kwani mashtaka yanayonikabili kwa mujibu wa sheria za nchi, hayana dhamana hasa mauaji yakukusudia, na unyang’anyi wa kutumia silaha!”
Inspekta Jamila, alitingisha kichwa chake juu chini, akiafiki maneno ya Mwaduga, kisha akamtupia swali la kijinga, lakini lenye maana kubwa kwa muulizaji!
“Sasa hapa upo kwa kesi gani? yakukutwa na silaha kinyume cha Sheria au kuhusishwa na uhalifu wa kutumia silaha?!”
Mwaduga alijibu, “Hapa natuhumiwa na mashitaka manne!“
“Shitaka la kwanza, kupanga njama ya kutenda kosa. Shitaka la pili, kufanya kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha. Shitaka la tatu kumiliki silaha kinyume cha sheria. Na shitaka la nne nashitakiwa kwa kosa la mauaji.”
Baada ya kusema hayo Mwaduga akaangua kilio. Inspekta Jamila akiwa makini zaidi akamuuliza tena Mwaduga swali lingine bila ya kujali kilio chake.
“Mada kesi imekujaje?! Au uliua mtu kupitia silaha zilizokamatwa na askari walikuta alama za vidole vyako, pamoja na ile silaha kuitambua?!”
Mwaduga akafuta machozi akaendelea kumjibu Inspekta Jamila.
“Katika uchunguzi wa Polisi ndani ya hii miezi miwili, wanadai walichogundua ni ile Bastola namba yake walipoifatilia, waligundua ni silaha iliyokuwa ikimilikiwa kihalali na mtu alietambulika kwa jina la Hamida Bartazal.”
“Sasa wale maaskari wakaniambia kwamba, huyo Hamida hivi sasa ni marehemu! Sababu ya kifo chake aliuwawa kwa kupigwa risasi na majambazi.”
“Na baadhi ya vitu vilivyoibiwa ilikuwa ni ile silaha iliyokutwa ndani ya gari yangu pale kwa Macheni. Ndipo nilipoelezwa, Kwa kuwa mimi ndiye niliyekutwa na ngozi, basi nitajua nyama ilipo!”
Inspekta Jamila alimuhoji vitu vingi Mwaduga, kiasi akajua wapi aanzie kufatilia mkasa ule mzito. Akaagana na Mwaduga kisha akashika njia akaenda zake akiwa na mawazo tele.
*****
Mkuu wa jeshi la polisi IGP akiwa ofisini kwake, alikuwa ameshika tama kwa mawazo.
“Mpenzi Samahani sana kwa hili ninalotaka kukwambia!” Hamida aliyasema maneno hayo, huku akiwa hana raha hata kidogo! bali anajilazimisha kuwa na furaha!
IGP aligundua hali hiyo na kumuuliza Hamida; “Vipi mbona unaonekana huna raha kabisa leo, ni mtu mwenye mawazo sana kulikoni?!”
Hamida alijichekesha kidogo na kusema, “Hapana nipo sawa tu, ila jana sikupata usingizi wa kutosha. Kwani nilikuwa najisikia vibaya sana, na kukupigia simu mtu na mkeo usiku umepumzika nikashindwa, nilichofanya nilimeza vidonge vya Diazapam nikaulazimisha usingizi! Nilipofumba macho kwa usingizi kulikuwa kumeshapambazuka!”
“Pole sana,je ulitaka kuniambia kitu gani?” IGP aliuliza.
“Nina mashaka kama nitachosema utaweza kukikubali!” Hamida aliyasema hayo huku akizidisha unyonge mara dufu.
“Sawa, sioni sababu ya wewe kuwa na mashaka, ikiwa kitu unachotaka kukisema ni cha kawaida!”
IGP alidadisi huku akiwa na shauku ya kutaka kujua jambo hilo!
“Kinaweza kikawa ni kitu cha kawaida kwangu, lakini kwako kikawa ni kitu kisichowezekana”. Alijibu Hamida.
“Sema nipo tayari kukisikiliza, kama kipo ndani ya uwezo wangu nitakupa”. IGP alimjibu hawara yake.
“Nashukuru kusikia hivyo ‘My Dear’. Kitu chenyewe ni, nahitaji kupiga picha na wewe ili unapokuwa kwa mkeo, na kwangu sura yako iwepo niwe naiangalia! Lakini pia Heshima ya kupiga picha na mtu mkubwa kama wewe, nadhani wanawake wenzangu wengi wangetaka kufanya hivyo!” Hamida alipokuwa akiyasema maneno hayo, alikuwa tayari yupo maungoni mwa IGP amemkumbatia!
“Duh! Sikutarajia kitu kama hicho, kwani nilidhani labda unataka nikununulie Gari!” IGP aliyasema hayo na wote wawili wakaangua kicheko cha chinichini.
“Mimi picha yako kwangu, ina thamani kuliko hata hiyo gari.”
“Sawa hilo lipo ndani ya uwezo wangu, piga picha utakazo!”
Kwa Camera ndogo Digital aina ya Olympus aliyokuwa nayo Hamida katika mkoba wake, akaitega Camera ile katika Automatic, na wakapata picha ya pamoja wote wawili wakiwa wanatabasamu.
IGP aligutushwa na simu yake ya mkononi iliyokuwa inaita, akaondosha mawazo yake na kuipokea ile simu.
*******
Inspekta Jamila alikuwa eneo la mikocheni jirani na Nyumba ya marehemu Hamida. akapiga hodi kwenye nyumba ya jirani, na kijana mmoja wa makamo, alifungua geti, nakumkaribisha ndani.
Baada ya kukaribishwa na kuketi, akajitambulisha na kuanza kumuhoji Bwana mmoja aliyemfahamu kama mwenye nyumba, aitwae Kiyarwenda Mwemezi.
Inspekta Jamila alianzisha mazungumzo baada ya kujitambulisha.
”Nipo hapa kwa ajili ya kufuatilia kifo cha aliyekuwa jirani yako Hamida, hivyo ninataka mchango wako wa mawazo, kama kuna chochote unachofahamu kuhusiana na kifo chake, na jinsi gani unavyomuelewa marehemu Hamida na tabia yake!”
Yule Jirani akafikiri kidogo kisha akajibu.
“Ooh ahaa Ok, mimi nipo hapa muda mrefu sana kabla marehemu Hamida hajanunuliwa nyumba hii na aliyekuwa marehemu mumewe!”
Inspekta Jamila alishituka kidogo akionekana kuwa makini zaidi, huku akimtupia swali la fadhaa jirani yule.
“Marehemu Hamida alikuwa na mume, na mazingira ya kifo chake yapoje huyo mumewe kadiri unavyofahamu?”
Yule jirani huku akimshangaa Inspekta Jamila alimjibu.
“Ndiyo marehemu Hamida alikuwa na mume aliyekuwa anaitwa Bartazal Halim, alikuwa Tajiri kiasi yule Bwana na mtu mkarimu sana! Amefariki miaka miwili iliyopita kwa kilichosemekana ni shinikizo la Damu!”
Inspekta Jamila alishusha pumzi, na akawa anamuangalia yule bwana kwa utulivu mkubwa uliojaa udadisi na umakini wa hali ya juu!
Na yule Jirani akaendelea.
“baada ya kifo chake, siku chache ndugu wa marehemu walijitokeza kudai mali za ndugu yao, lakini ulitokea mshangao wa mwaka!
kwani miezi mitatu nyuma marehemu Bartazal inasadikiwa alimuandikisha mali zake zote mkewe Hamida!
Ndugu wa marehemu hawakuridhika na jambo hilo hata kidogo! kwani katika uhai wake, marehemu hata siku moja hakuwahi kuwaambia ndugu zake kama amemuandikia mkewe mali zote!
Lakini pia kaka yao hakuwahi kupata kuugua shinikizo la Damu katika maisha yake ya miaka hamsini na ushee!
Ila Daktari katika ripoti yake alisema, marehemu aliona au kusikia jambo la kushitua sana, na ndiyo ikapelekea kupata shinikizo la Damu nakusababisha kifo chake!”
Inspekta Jamila huku akimuangalia usoni jirani yule, akasema huku akiwa hana Raha hata kidogo!
“Nimekuja hapa kujua namna kifo cha Hamida kilivyotokea! Ila haya unayonipa nayo ni taarifa inayopaswa kufanyiwa kazi! Lakini je? Wewe uliyajuaje? Yote haya!”
Jirani wa Marehemu Hamida akamjibu.
“Marehemu Bartazal alikuwa ni rafiki yangu sana, na hata ndugu zake walipokuwa wakija kumuona, lazima aliwaleta kwangu au mimi kwenda kwake.
Na hao ndugu zake ndiyo waliokuwa wakinipa taarifa hizi zote!”
Inspekta Jamila akamtupia swali lingine Bwana Yule.
“Nikitaka kuwaona hao ndugu zake marehemu Bartazal naweza kuwaona wapi?”
Jirani yule alimkatisha tamaa kabisa jibu lake alipojibu.
“Marehemu Bartazal hana ndugu kwa sasa hapa Dsm, kwani baada ya mazishi, na kumalizika Arubaini, alikuja ndugu yake mmoja na kunieleza kwamba anasafiri, anakwenda kuishi Marekani. Yeye na familia yake, na nikawasindikiza hadi Uwanja wa ndege, na baada ya ndege kuruka mimi ndiyo nikaondoka!
Ila yule ndugu yake wa kike, nina mwaka sasa sijui wapi alipo, na kama yupo hai, au amekwishakufa. Kwa hapa nchini walikuwa wanaishi Arusha.”
Inspekta Jamila huku akitingisha kichwa kwa majibu yale muhimu katika kesi ile akamtupia swali linguine.
“Sawa. Turudi kwa marehemu Hamida, je baada ya kifo cha mumewe mliendelea kuwa majirani wema?”
Yule Jirani bila ya kusita wala kuuma maneno akajibu swali lile, huku akitikisa kichwa kwa masikitiko.
“Marehemu Hamida alinichukia ghafla sana akidai kwamba, mimi na ndugu wa marehemu mumewe, tuna njama za kumnyang’anya mali zake za urithi wa marehemu mumewe. Hivyo akanichukia toka siku ile!”
Inspekta Jamila akiwa na mawazo tele akamuangalia tena yule bwana kuanzia juu hadi Chini,kisha akamtupia swali jingine huku akiangalia ile “Tape Recorder” yake kama inafanya kazi yake sawa sawa!
“Sasa nataka kufahamu jambo lingine kutoka kwako, baada ya marehemu Bartazal, nani alikuwa mwanaume anayelala na kuamka na Hamida? na je tabia yake ilibaki kuwa ileile kama alipokuwa na marehemu mumewe au ilibadilika?!”
Jirani yule huku akionyesha kuchoshwa na kukerwa na maswali alijibu.
“Nikianza na Tabia, kwa kweli ilibadilika. Kwani alianza tabia za ulevi na kurudi usiku mwingi! Na kuhusu mwanaume, kwa kweli sina hakika na hilo, kwani mie huwaona wanaume tofauti tofauti. Na asilimia kubwa ni vijana wenye uwezo mkubwa kifedha, kwani magari yanayoingia humo ndani ni ya kifahari tupu!”
Inspekta Jamila alivutiwa na habari hiyo, kiasi ilimfanya akae vizuri na kumuuliza.
“Unaweza kuzikumbuka namba za magari zilizokuwa zikiingia na kutoka mara kwa mara kwa marehemu Hamida?!”
Jirani yule akionyesha kuchoshwa na maswali ya mfululizo alijibu.
“Mh kwa kweli huo ni mtihani, kwani kukaa kuchunguza namba za magari ya watu! Hapana hilo sikumbuki hata kidogo.”
-
Inspekta Jamila akamuwahi kwa swali lingine tena, safari hii akimkazia macho yake laini, kiasi badala ya kutisha yaliongeza urembo wake!
“Sawa na kifo cha Hamida, kilitokea baada ya kuvamiwa na majambazi nakupigwa risasi ya kichwa iliyotoa uhai wake. Je? Hufikirii ni jambo la kupangwa kwa ajili ya kisasi cha marehemu mumewe?”
Jirani yule sasa akiwa amechoka kabisa kujibu maswali mfululizo alijibu kwa mkato.
“Sina hakika, hiyo ni kazi yenu polisi kujua!”
Inspekta Jamila aliendelea kumuhoji jirani yule hadi aliporidhika kwamba amepata taarifa zote alizozitaka, akaagana na bwana Yule, huku akichukua namba ya simu ya jirani yule, akaondoka.
*******
Siku tatu Baadae! Ikapatikana taarifa ya ajali mbaya iliyochukua uhai wa mtu
katika Eneo la Bunju, kwenye Daraja la Mto Mpiji, mpakani mwa Mkoa wa Dsm na Mkoa wa Pwani Wilaya ya Bagamoyo.
Mtu aliefariki katika ajali ile, alitambuliwa kuwa ni Bwana Kiyarwenda Mwemezi, yule jirani yake marehemu Bartazal na marehemu Hamida aliyeongea na Inspekta Jamila siku tatu nyuma.
Alikutwa na kitambulisho chakupigia kura kwenye pochi yake, pesa tasilim shilingi elfu hamsini, iliyosalimika kuibiwa na vibaka labda, baada ya askari wa Usalama kufika eneo la tukio muda mfupi tokea ajali ile itokee, ambayo gari iliacha njia na kuingia mtoni ikichoma chini kwenye maji machache ya mto, yaliyokuwa yanaelekea Baharini!
Simu ya marehemu haikupatikana kwenye eneo la tukio. na hata Inspekta Jamila alipokuwa anaipiga tena na tena jibu lilikuwa ni lilelile.
“NAMBA UNAYOPIGA KWA SASA HAIPATIKANI TAFADHALI JARIBU TENA BAADAE!!”
Inspekta Jamila alichanganyikiwa kupita kiasi huku akizidi kupata shaka kwamba Kifo cha Hamida inawezekana ikawa ni kisasi cha marehemu mumewe! Lakini ikiwa ndugu hawapo je ni nani tena anaeendeleza mauaji haya?!
Na akiwa marehemu Hamida kweli alimuuwa mumewe kwa njia moja au nyingine, kwa nini afanye hivyo? Kama ikiwa ni kutaka mali mbona alishaandikishwa na mumewe?! Kijasho chembamba kikamtoka Inspekta Jamila!
****
Inspekta Jamila akiwa nyumbani kwa marehemu Hamida, akiwahoji ndugu wa marehemu Hamida wanaoishi mle ndani, kisha kama mtu aliegutushwa na kitu, akataka aletewe Albamu zote za picha za marehemu Hamida. Wale ndugu wakasema.
“vitu vyote vipo chumbani kwa marehemu.”
yule mwenyeji wake alikwenda katika chumba cha marehemu Hamida na kurudi na picha za marehemu Hamida zilizokuwa katika albam nne na kumkabidhi
Inspekta Jamila.
Inspekta Jamila alizipitia Albam zile moja baada ya moja, alipofika katika
Albam ya Tatu iliyoonekana ni mpya kidogo tofauti na zile zilizopo pale, ilimvutia kuitazama Inspekta Jamila, na picha ya tatu toka aanze kuifungua ile Albam alikutana na kijana mmoja wa kiume, aliyekuwa ameshika Glass ya Bia akimnywesha marehemu Hamida.
Inspekta Jamila Akaiangalia kwa makini kisha akaigeuza nyuma na kukuta imendikwa tarehe iliyopigwa ile picha na mahali ilipopigwa tu! Haikuwa na jina la yule mhusika katika picha ile wala la Hamida!
Inspekta Jamila akaichomoa na kuitumbukiza kwenye ‘HAND BAG’ yake na kuendelea kufungua picha zingine. Mara! hakuyaamini macho yake alipokutana na picha ya Bosi wake kwenye Albam ile, akiwa anapata chakula cha jioni katika Mgahawa mmoja maarufu, akiwa na Marehemu Hamida!
Inspekta Jamila akashusha pumzi ndefu huku akifikiri kwa undani zaidi kwani haelewi uhusiano wa mkuu wake wa kazi na marehemu Hamida, hata wakapiga picha ya pamoja. Na ataanzaje kumuhoji mkuu wake wa kazi kuhusu picha yake kuwa katika Albam ya marehemu Hamida, na hasa ukizingatia yeye Inspekta Jamila, hakukabidhiwa kesi hiyo na yeye anapeleleza kwa siri ili kupata ukweli wa mambo! Kwa mujibu wa BARUA KUTOKA JELA.
Mwisho ile picha nayo akaichukua na kuiweka ndani ya mkoba wake, akaendelea kupekua picha zingine. Kwa mara nyingine akapatwa na mshtuko wa mwaka, pale alipomuona Dokta Masawe akiwa amepozi na marehemu Hamida! Ndani ya gari nyekundu, aina ya TOYOTA CALDINA! na ni picha ambayo haikupigwa muda mrefu sana toka Hamida atoke kuwa KIZUKA. Kwa mujibu wa maandishi yaliyokuwa nyuma ya picha ile, tarehe, mwezi na mwaka. inavyosomeka!
Dokta Masawe ni daktari bingwa na maarufu kwa kuunga mifupa, na viungo vya mwanaadamu, anaefanya kazi katika hospitali ya rufaa ya Muhimbili kitengo cha Moi.
Inspekta Jamila akaichomoa na ile picha na kuitumbukiza ndani ya kibegi chake maarufu kwa jina la kipima joto, na alipoiangalia ile Albam ya nne haikuwa na picha za maana kwake. Hivyo Inspekta Jamila akawaambia wale wenyeji wake.
“Nimechukua picha tatu kwa upelelezi zaidi. Baada ya kukamilisha zoezi zima nitazirejesha!
Nashukuru kwa ushirikiano mlionipa, mungu akipenda nitarudi tena siku nyingine.”
Akachukua namba ya simu ya yule mdogo mkubwa wa marehemu Hamida aliejitambulisha kwake kwa jina la Neema, Akaaga na kutoka eneo lile huku akiwa na msongamano wa mawazo ukitembea katika kichwa chake, nakujuta kujiingiza katika kesi ile ambayo, inaonekana ni kubwa kuliko alivyofikiri yeye!
*******
Maeneo ya Mburahati Barafu, bwana Masudi akiwa amekaa na mkewe anakunywa chai, mara akasikia hodi. Naye akamwambia mkewe akamsikilize mgeni kwa kuwa ilikuwa ni sauti ya kike!
Mke wa masudi, anatambulika sana maeneo yale kwa jina la Mama chapati, kwa umaarufu wake wa kuchoma chapati ambazo ili uzipate chapati zake, itakubidi mtu udamke asubuhi na mapema sana. Kwa wale wenye usingizi wa pono, watazisikia kupitia kwa watu waliozinunua na kuzila!
Yule mwanamke mnene na mrefu wa wastani aliinuka, akafunga khanga yake vizuri kifuani na kufungua mlango.
Akakutana uso kwa uso na mwanamke mmoja mwenye sifa zote za kuitwa mrembo. Yule mgeni, alimsalimu mwenyeji wake, kisha akamuuliza.
“Samahani Dada, Bwana Masudi nimemkuta?”
Mke wa Masudi akajibu. “Ndiyo umemkuta na mimi ndiye mkewe, tukusaidie nini, na unashida gani na mume wangu?!”
Mke wa Masudi aliuliza maswali yaliyojaa wivu tele! “Nashukuru kukufahamu kuwa wewe ndiye mke wa Bwana Masudi, pia ninafurahi kusikia nimemkuta Bwana Masudi, kwani mguu huu ni wa kwake!”
Alijibu Yule mgeni bila ya khofu yoyote huku akijiamini nakumtazama yule mwanamke machoni bila kupepesa macho!
Kitendo kilichomshangaza sana mke wa Masudi.
Na mara Masudi akatokea pale, baada ya kusikia maneno ya wale wanawake wawili. “Karibu”,
Bwana Masudi akatamka, huku akimtazama kwa umakini yule mwanamke mwenye kutetemesha wanaume wengi kwa urembo wake.
“Aksante bila shaka wewe ndiye Bwana Masudi?”
Masudi akaitikia kwa kichwa, na yule mgeni akaendelea.
“Mimi ni mgeni wako na nimefurahi kukukuta, kiasi najiita ni mwenye Bahati kwa siku ya leo!”
Mke wa Masudi akamtazama mumewe huku akiwa amekasirika vibaya sana, akamwambia mumewe.
“Hivi huo umalaya wako unauleta hadi nyumbani? Umeona huko nje hakutoshi mpaka uniletee nyumbani wanawake zako? Tuseme huwaambii kama umeowa mpaka wakufate nyumbani tena asubuhi?!”
Yule mgeni akapigwa na butwaa! Akimsikitikia Mwanamke mwenzake alivyokuwa hajiamini!
Masudi akiwa ametaharuki kwa maneno ya mkewe pia akiona vibaya dhana mbaya ya mkewe, hatimaye akamwambia mkewe.
“Mke wangu vibaya namna hiyo. Huyu ni mgeni na hujui yupo hapa kwa ajili gani, hivyo si busara kutoa lugha ya namna hiyo! Msalie mtume mwanamke heh!”
“Ukiona hivyo huaminiki kwa mkeo ndiyo maana anakuwa hivyo”.
Akajibu Yule mgeni huku akitabasamu! Kitu ambacho kilimzidisha hasira mke wa Bwana Masudi mara mbili ya mwanzoni!. Naye Bwana Masudi akiwa anamtazama yule mwanamke huku akishangaa kwa ujasiri anaouonyesha kwenye nyumba yao.
“Okey mimi ninaitwa Inspekta Jamila kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, nipo hapa kwa ajili ya mahojiano machache tu na wewe Bwana Masudi, kuhusu kesi inayomkabili jirani yako na Swahiba wako mkubwa Bwana Mwaduga Dingo.”
Inspekta Jamila aliyasema hayo huku akionyesha kitambulisho chake.
Mke wa Bwana Masudi akashika kichwa, kisha akakaa chini kwa hofu aliyoipata baada ya kuona mtu aliyekuwa akimtilia mashaka ya wizi wa mumewe, kumbe ni Askari mpelelezi.
Bwana Masudi nae macho yalimtoka pima akiwa hakutegemea kitu kama kile kutokea.
“Karibu Inspekta na samahani kwa yote yaliyojitokeza.” Hatimae Masudi akajibu.
Inspekta Jamila huku akiwa amemnyooshea mkono wake wa kulia, akiashiria kwa kiganja chake kuwa ameisamehe ile hali, akamwambia.
“Usijali ni mambo ya kawaida tu hayo, nishakutana na changamoto zaidi ya hizi nikiwa nipo kazini!”
Baada ya kuketi hatimaye mke wa Bwana Masudi alipata kauli ya kusema.
“Afande nisamehe kwa kukujibu vibaya.”
“Usijali, Usijali mambo ya kawaida hayo, ila mwanamke lazima ujiamini.”
Inspekta Jamila aliyasema hayo, Huku akimgeukia Bwana Masudi. Akatoa kalamu na kijitabu chake akiwa tayari kwa mahojiano!
“Bwana Masudi unakumbuka nini kilichomtokea jirani yako Mwaduga? Na mara ya mwisho kuonana na jirani yako akiwa huru? Ilikuwa katika mazingira gani na wapi?!”
Inspekta Jamila akaanza kwa maswali mfululizo.
Bwana Masudi akiwa katika hali ya huzuni iliyochanganyika na hofu, akafikiri kidogo kisha akasema.
“Nakumbuka kiasi cha miezi miwili nyuma nikiwa maeneo ya Sinza Madukani, katika mihangaiko yangu ya kila siku niliona gari ya jirani yangu anayoiendesha, na nilipomwangalia Dereva anayeendesha nikaonana uso kwa uso na Mwaduga!
Wote wawili tukatabasamu, na Mwaduga akapaki pengeni gari yake.
Nilipofika Karibu na gari ilipopaki, wakatokea jamaa watatu wakiwa wamebeba begi na viatu wameshika mikononi kama wamachinga wakaingia ndani ya gari, nami wakati huo nilishafika pale kwenye gari. Wale jamaa mmoja aliepanda mbele akasema tunazo Elfu tatu tupeleke Bar ya Macheni Magomeni! Mwaduga akanambia tutaongea nyumbani akaitoa gari nakuiweka barabarani huku anatabasamu!”
Inspekta Jamila akamkazia macho Bwana Masudi huku akiandika kwenye kitabu chake kidogo na akadakia kwa swali!
“Umesema wale jamaa watatu walipanda gari wewe ukiwaona na si kama Mwaduga alitoka nao sehemu kabla ya pale, Je?! Kwa nini basi alikuwa anatabasamu baada yakuwapakia wale jamaa? Na kama alisimama kwa ajili yako mbona alichosimamia hamjaongea yeye akaondoka?“
Bwana Masudi akajibu; “Wale jamaa wamepanda gari yake na mimi nikiwa pale, sio kama alikuja nao kwenye gari. Labda lililomfanya akatabasamu, ninahisi kwa vile yeye anapaki kule magomeni usalama na alikuwa anarudi tupu, sasa amepata abiria wanaomrudisha kijiweni kwake kwa shilingi 3000/ mtu yeyote angefurahia bila shaka!”
“Sawa je utapowaona tena watu wale unaweza kuwakumbuka?! Na unaweza kunipa wasifu wao namna walivyo?! Au hata nguo walizozivaa siku ile?”
Inspekta Jamila alimuuliza Masudi kwa shauku. Na Masoudi akajibu.
“Kwa kweli yule mmoja aliepanda mbele namkumbuka kwa sura. Jamaa ana kithethe anapoongea, kwani hata neno tunazo Elfu tatu, yeye alitamka TUNADHO ELFU TATU! Wale wengine wawili sikuwakariri sura zao sawasawa kwani gari ilikwisha ondoka! Ama nguo alizovaa yule jamaa aliepanda mbele, alivaa suruali ya jinzi na fulana moja nzuri sana iliyokuwa imeandikwa MKIMBIZI ikiwa na picha ya mwana dada mmoja akiwa kama anakimbia! Ile jinzi ilikuwa na Rangi nyeusi na fulana ya rangi nyeupe.”
Inspekta Jamila akamuhoji Masudi mambo mengi kiasi akaridhika kwa hatua aliyopiga. Na kiasi alianza kupata Mwanga kuwa, Mwaduga hakuwa anajua chochote katika mkasa unaomkabili, lakini ataihakikishiaje serikali ili ielewe kile anachosema?! Na kama Mwaduga si muhusika, je nani ataesimama akiwa ndiye muhusika halisi?
Inspekta Jamila. Akaagana na Masudi huku wakipeana mkono wa kwa heri yeye na mkewe, ambae sasa alikuwa ni mtulivu na mwenye nidhamu ya hali ya juu!
*****
Wapelelezi wawili walikuwa wamekaa kwa pamoja wakijadili hali ya upelelezi wao walioufanya katika kesi inayomkabili Dereva Taxi Mwaduga Dingo, kwani kesi ya mauaji inayomkabili, sasa jalada lake, upelelezi umeshakamilika, na mwendesha mashtaka wa serikali anatarajia kulipeleka jalada mahakama kuu kwa ajili ya kesi kuanza kusikilizwa. Baada ya kutajwa mara kadhaa katika Mahakama ya hakimu mfawidhi ya Kisutu, Mahakama ambayo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji kwa mujibu wa sheria za nchi.
Afande Kubuta ambae ndie mpelelezi, aliekabidhiwa kupeleleza kesi zinazomkabili Mwaduga Dingo, akiwa na mpelelezi mwenzake Afande Magane, walikuwa wanalipitia lile faili kwa kituo, ili liwasilishwe Mahakama kuu kwa kusikilizwa.
Afande Kubuta alianzisha mazungumzo. “Yule kijana kwa jinsi nilivyo muhoji na kumpa kibano lazima angesema kila kitu yule, lakini yule kijana kama ni sugu basi yule ni mwalimu wao! Kwani katika mkono wangu, haijawahi kutokea mualifu nimuweke katika kiti moto kisha asinieleze ukweli, ndiyo kwanza yule kijana amefanikiwa! Ameharibu CV yangu yule!”
Afande Magane akasema: “Inawezekana yule ameshawishiwa na wale jamaa akaingia katika mkumbo kwa tamaa ila wale jamaa hawajui wala nini!”
Afande Kubuta nae akasema. “Tulipokwenda kumpekua, nyumbani kwake hatukukuta vitu vya maana sana, ila kulikuwa kuna Tv moja aina ya Sony nchi 14 mpya kabisa, na nilipohitaji stakabadhi iliyonunulia Tv ile, nikahisi kuwa yule kijana anahusika kwa namna moja au nyingine. Kwa sababu stakabadhi ile tarehe yake ilikuwa inaonyesha kuwa, Tv ile imenunuliwa siku moja baada ya mauwaji ya Hamida kutokea! Na kwa kuwa Silaha ya Marehemu Hamida amekutwa nayo yeye, kisha Tv yake imenunuliwa siku moja baada ya kifo kile, hii wala haihitaji Digirii kutambua kwamba baada ya kijana yule kushiriki katika tukio lile la mauwaji, mafao yake ndiyo amenunulia Tv”
Hivyo Wakiwa katikati ya Mjadala ule simu ya Mkononi ya Afande Kubuta iliita na alipoiona namba ya simu iliyokuwa inaita, moyo wa Afande Kubuta uliruka sarakasi na kuipokea simu ile.
“Ndiyo Afande, sawa mkuu, nimekusoma Afande!” Kisha ilikatwa simu ile.
Afande Magane akamuuliza.
“Vipi ni mkuu wa kituo huyo aliepiga simu hiyo?!”
Afande Kubuta akamjibu “Hapana huyo ni IGP bwana, na sijawahi kupigiwa simu hata mara moja na IGP”
Afande Kubuta akamueleza yote aliyoongea bosi wao.
Afande Magane akashangaa sana kusikia habari hiyo, na akasema.
“Bila shaka kuna mtu amekwenda kwa IGP anayehusiana na mtuhumiwa, na kuongea na IGP! Sasa kama hivyo ndivyo basi kesi hii rafiki yangu, inabidi uwe makini sana. Kwani wewe ndiye mpelelezi wa kesi hii mwenye Jalada lake! Sisi wengine tunapewa amri tu, Fatana na afande fulani kwa upekuzi na majadiliano tunafanya hivyo! Duh hii hali sasa ishakuwa pevu, je? unayo ripoti iliyokamilika ya upelelezi wa kesi hii sasa? Kwani ndiyo inatakiwa ili ionekane bila shaka afande kama angetaka kujua angeuliza umefikia wapi kwenye upelelezi wa kesi hii. Ila hapa naona kuna kitu cha ziada kutoka kwa Bosi kwani Photo Albam na Note Books vya marehemu yeye vya nini? Okay sasa mimi naona twende Mikocheni kwanza kutekeleza amri ya Bosi kisha uvipeleke kama alivyoagiza, kisha tusikilize atakwambiaje kwani tunaweza kuumiza vichwa kumbe mambo yenyewe ni shwari tu!”
*******
Afande Kubuta na Afande Magane walibisha hodi nyumbani kwa marehemu Hamida, walipofunguliwa mlango wakajitambulisha ikiwa ni pamoja na kutoa vitambulisho vyao vya kazi.
Wakakaribishwa ndani, walipofika ndani wakaeleza walichokiendea pale. “Kama tulilvyokwisha jitambulisha, tupo hapa kikazi hivyo tunahitaji Photo Albam zote za marehemu Hamida pamoja na vitabu vyake vya kumbukumbu.”
Yule dada aliyewapokea akaanza kuvitafuta vitabu vyake vya kumbukumbu marehemu Hamida chumbani kwake kwani “photo albam” zilikuwa mezani chumbani mle.
Yule dada akawakabidhi “photo albam” nne afande Kubuta akazichukua na kuziweka kwenye mfuko wake wa ngozi alioushika mkononi, akifarijika angalau anachokitaka Bosi wake kutoka kwenye nyumba ile, kimoja amekwisha kipata. Iliwachukua kama nusu saa kuja kukiona kitabu cha kumbukumbu cha marehemu Hamida. Yule dada aliyejitambulisha kama mdogo wa Hamida, anayejulikana kwa jina la Neema, akawaambia askari wale.
“Jana alikuja afande mwenzenu wa kike aliyejitambulisha kwa jina la afande Jamila, amechukua picha tatu kutoka katika albamu hizo, na ameahidi kuzirudisha mara baada ya kukamilisha upelelezi wenu!”
“Whaat?!”
Afande Kubuta na mwenzake afande Magane walijikuta wakisema kwa pamoja huku wakiwa hawaamini masikio yao kwa kile walichokisikia kutoka kwa Neema!
“Umesemaje?!” Afande Kubuta akamuuliza Neema.
“Mbona mmeshituka sana, ina maana hamna taarifa za picha hizo kufika ofisini kwenu? Mimi nimejua mmekuja kuchukua nyingine ili mkamilishe huo upelelezi wenu!” Neema badala ya kurudia kauli yake, akatoa maneno yalioonyesha kumshangaza, kwa namna kesi ile inavyoshughulikiwa!
Hatimaye akairudia tena kauli yake, sasa akiwa makini zaidi ya mwanzo.
“Juna alikuja afande mwenzenu wa kike, aliyejitambulisha kwa jina la afande Jamila. Amechukua picha tatu kutoka katika albam hizo, na ameahidi kuzirudisha mara baada ya kukamilisha upelelezi wenu.”
Neema alirudia kauli ile huku akiwatazama machoni maafande wale wawili waliopigwa butwaa ya mwaka!
“Samahani dada, huyo afande Jamila alipokuja alikwambia anatokea Kituo gani?”
Aliuliza afande Kubuta. “Na alikuonyesha Kitambulisho?” Akaongeza swali afande Magane.
Sasa ilikuwa zamu ya Neema kupigwa na butwaa.
“Yaani mnataka kuniambia, kwamba afande Jamila hamumtambui?” Aliuliza Neema huku akivuta tafakari na kuwa makini zaidi.
“Jibu swali mwanamke”, afande Kubuta akasema huku akiwa amechanganyikiwa kwa kauli ya neema.
“Jibu maswali mwanamke.” Afande Magane akadakia na huku akiendelea kusema. “Hii ni kesi ya mauaji hivyo usije kuleta mzaha umesikia?”
Neema aliitikia kwa kutikisa kichwa. Kisha akajibu, “Alipokuja hapa jana alijitambulisha yeye ni askari polisi na akatoa kitambulisho chake kama nyinyi mlivyofanya. Ila hakusema ametokea kituo gani cha polisi! Akataka “photo albam” kama nyinyi mlivyotaka, nami nikampa na baada ya kuzipekua, akachomoa picha tatu akatia kwenye mfuko wake kama nyinyi mlivyochukua hizo albam na kutia katika mfuko wenu. Ila yeye hakutaka kitabu cha kumbukumbu, baada ya kupata picha zile akaaga na kuondoka.”
Afande Kubuta akamuuliza “je alikuonyesha picha alizochukua?”
“Hapana” Neema akajibu.
“Ila unazitambua picha zilizokosekana katika albam hizo?”
Afande Magane akamuuliza Neema huku akimkazia macho.
“Hapana kwani mimi nimekuja hapa ulipotokea msiba, kabla ya hapo nilikuwa siishi hapa, hivyo picha za marehemu dada zote alizopiga ukiondoa za harusi yake ambazo nimeziona nyingine zote sizijui.” Akamaliza Neema huku akifuta machozi yaliyoanza kumtoka, labda baada ya kukumbuka picha zilizomuonyesha dada yake akiwa katika maisha yake ya ndoa!
“Sawa alikuachia namba za simu huyo afande Jamila?” Hatimaye akauliza afande Kubuta.
“Hapana hakuacha, ila alichukua namba yangu ya simu na kusema angenipigia pindi ambapo angelihitaji msaada kutoka kwangu.”
Ama kwa hakika askari wale walichanganyikiwa sana kwani kila kitu walichokitarajia kuwasaidia kumtambua huyo afande Jamila waliambulia jibu la hapana! Ama kweli walikuwa wamepigwa bao la kisigino. Mwisho wa yote wakaacha namba zao za simu na kumwambia Neema.
“kama atakuja tena huyo afande Jamila muulize anatokea kituo gani, na unipigie simu mara moja. kwani mimi ndiye mpelelezi katika kesi hii. Hivyo mtu yeyote atakayejihusisha na kesi hii, lazima mimi nimtambue.”
Mwisho wakaaga na kuondoka.
*******
ITAENDELEA

0 Reviews